Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

Washiriki wa Mradi wa Kimataifa Kukomesha Maradhi ya Shurua Ulimwenguni – ikijumlisha Shirika la Wakf kwa UM, pamoja na mashirika ya UM juu ya afya, WHO, na maendeleo ya watoto, UNICEF – yameripoti kwamba vifo vya maradhi ya shurua miongoni mwa watoto wa kimataifa, vimeporomoka kwa asilimia 74, kutoka idadi ya vifo 750,000 katika 2000 na kuteremka kufikia jumla ya vifo 197,000 katika 2007.

Alkhamisi asubuhi KM Ban Ki-moon alizungumza kwa simu na Raisi Kgalema Motlanthe wa Afrika Kusini juu ya matatizo ya kiutu yaliopamba Zimbabwe sasa hivi. Kwenye mazungumzo hayo KM alitilia mkazo umuhimu wa Umoja wa Mataifa, na washiriki wengine wakimataifa, kuharakisha mchango wa misaada ya kihali kuihudumia Zimbabwe kidharura kukidhi mahitaji ya kimsingi ya raia. Vile vile alipendekeza kuchukuliwa hatua za pamoja, halan, katika zile operesheni za kujaribu kukomesha maradhi ya kipindupindu, yaliofumka nchini, yasije yakasambaa na kuhatarisha maisha ya umma wa mataifa jirani.

Shirika la UM juu ya Cote d’Ivoire (ONUCI) limeripoti kuunga mkono mafanikio ya karibuni, ya kihistoria, ambapo usajili na utoaji wa vitammbulisho kwa raia, kabla ya uchaguzi ujao wa uraisi ulikamilishwa. Ijapokuwa kulitukia ucheleweshaji mdogo katika huduma hizo, ikichanganyika na mapigano machache ya hapa na pale katika miezi ya karibuni, matayarisho hayo yalifanikiwa kuwapatia watu milioni mbili vitambulisho rasmi vitakavyowezesha asilimia kubwa ya raia kupiga kura bila matatizo.

Mkutano wa kutia sahihi Mkataba wa Kupiga Marufuku Vijibomu vya Mtawanyo vya Klasta umekamilisha shughuli zake kwenye mji wa Oslo, Norway Alkhamisi ya leo, ambapo zaidi ya mataifa 100 yaliridhia kutotumia, au kutengeneza, na wala kuhamisha kwenye maeneo mengine zile silaha za vijibomu vya mtawanyo vya klasta. Kati ya serikali 100 zilizohudhuria mkutano wa siku mbili Oslo, mataifa 94 yalitia sahihi Mkataba, nchi 4 ziliridhia Mkataba wakati taifa moja lilituma ombi la muda la uthibitisho wake. Mkataba sasa upo tayari kutiwa sahihi na Mataifa Wanachama yote ya UM, na warka utawekwa Makao Makuu mjini New York ukisubiri sahihi za kuuthibisha kuwa chombo rasmi cha sheria ya kimataifa. Ridhaa ya Mataifa Wanachama 30 inahitajika kuugeuza Mkataba kuwa chombo rasmi cha sheria ya kimataifa.