Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM unaadhimisha Siku ya Kimataifa Kukomesha Udhalilishaji wa Kijinsiya

UM unaadhimisha Siku ya Kimataifa Kukomesha Udhalilishaji wa Kijinsiya

UM na mashirika yake kadhaa ulimwenguni yanaiadhimisha siku ya leo kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Kukomesha Utumiaji Nguvu dhidi ya Wanawake.

KM Ban Ki-moon alisema kwenye risala yake kuiadhimisha siku hii ya kuwa sisi sote tunawajibika kuongeza juhudi zetu kwenye utekelezaji hakika wa sheria za kukabiliana na tabia ovu ya wale wanaodhalilisha wanawake bila kukhofu adhabu. Kadhalika, KM alitoa mwito unaoitaka jamii ya kimataifa kukithirisha mchango wa fedha zinazohitajika kuhudumia bora waathiriwa na wanawake walionusurika na mateso ya kijinsiya.

Kwenye risala alioitoa kuihishimu Siku ya Kukomesha Utumiaji Nguvu dhidi ya Wanawake, Kamishna Mkuu wa UM juu ya Haki za Binadamu, Navi Pillay, yeye kwa upande wake aliyahimiza Mataifa Wanachama kuhakikisha wanawake wanashirikishwa kikamilifu kwenye mijadala yote inayohusu mapatano ya amani, kwa sababu imethibitika wazi kabisa kwamba kwenye mazingira ya uhasama na mapigano wanaodhalilishwa na kuathirika zaidi na mateso, ni wanawake na watoto wa kike, umma ambao mara nyingi hunajisiwa kimabavu, vitendo karaha ambavyo hutumiwa na wapiganaji kama silaha ya vita. Pillay alipongeza uamuzi wa Baraza la Usalama kutambuwa vitendo vyote vya kunajisi wanawake, pamoja na vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia, ni makosa ambayo yameambatanishwa na uhalifu dhidi ya utu na mauaji ya halaiki, na ni sawa na jinai ya halaiki. Kwa hivyo Kamishna Mkuu wa UM juu ya Haki za Binadamu amehimiza nchi wanachama kuimarisha sheria za kizalendo zinazohitajika kuwapatia wanawake hifadhi bora dhidi ya unyanyasaji na udhalilishaji wa kijinsia.