Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale (Taarifa za kusoma)

Hapa na pale (Taarifa za kusoma)

Kikao cha 63 Baraza Kuu la UM kiliongozwa na Raisi wa mwaka huu Miguel d’Escoto Brockmann wa Nicaragua. Kabla ya Raisi wa Baraza Kuu kufungua rasmi majadiliano ya wawakilishi wote, KM wa UM Ban Ki-moon alihutubia kikao kwenye ukumbi wa Baraza Kuu ambapo aliwasilisha taarifa ya mapitio ya mwaka kuhusu shughuli za UM ulimwenguni. Baada ya hapo Raisi Miguel d’Escoto alihutubia wawakilishi wa Mataifa Wanachama 192, na alifuatiwa na Raisi Luiz Inácio Lula da Silva wa Brazil ambaye taifa lake, kwa kulingana na mila za UM, huwa ni taifa la awali kuongoza majadiliano ya jumla kwenye Baraza Kuu.

Raisi George W. Bush wa Marekani kwenye taarifa alioitoa mbele ya Baraza Kuu alisema imethibitika kihakika kwamba UM, hivi sasa, ndio ni chombo muhimu kinachohitajika na kinachotakiwa kukabiliana, kwa mafanikio, na vitisho vya ugaidi wa kimataifa, kwa sababu taasisi hii yenye wahusika wingi ndio yenye uwezo pekee wa kuwasilisha enzi yenye ustawi na usalama imara ulimwenguni. Alisisitiza kwamba mafanikio kwenye vita dhidi ya ugaidi yanategemea ushirikiano miongoni mwa mataifa katika kuzuia mashambulio ya ugaidi kabla hayajatukia, ili kujiepusha na majuto ya baadaye. Alisema “utumwa, uharamia na ugaidi ni mambo yasiofaa kabisa kuwepo katika dunia ya sasa.”

Raisi wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy, akizungumza kwa niaba ya Umoja wa Ulaya, yeye alisema kwenye risala yake kwamba uwanachama wa Baraza la Usalama pamoja na katika taasisi muhimu nyengine za kimataifa unahitajia kupanuliwa haraka ili kuuwezesha ulimwengu kufanikiwa kukomesha matatizo hatari yaliokabili umma wa kimataifa. Raisi Sarkozy alitilia mkazo taasisi hizi za kimataifa ni lazima ziwe na “uwazi unaoeleweka, na uwakilishi wa wote, na kwa madaraka yenye nguvu itakazozipatia taasisi hishima na imani ya kimataifa”, hali ambayo itasaidia kusulushiha mizozo sugu kadha wa kadha, mathalan, yale matatizo yaliotukabili kwa sasa kwenye soko za fedha za kimataifa.

Raisi Jakaya Mrisho Kikwete wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika aliliambia Baraza Kuu kwamba nchi za Afrika zimeonyesha maendeleo muhimu katika utekelezaji wa mfumo wa kidemokrasia, kuhishimu haki za binadamu, kukabiliana na ulaji rushwa na pia katika kuimarisha uchumi wao. Alisema Afrika ina matumaini ya kutia moyo kwa siku za usoni. Alisisitiza Afrika ni “bara lisio na mategemeo kama inavyodhaniwa na baadhi ya mataifa.” Alisema kuna mafanikio mengi ya kutia moyo katika Afrika, mathalan, kuna utulivu wa mazingira ya kisiasa, amani imetanda takriban katika mataifa yote, isipokuwa machache tu, wakati uchumi wa nchi nyingi za Afrika unaashiria ustawi mzuri. Kadhalika, Raisi Kikwete alitahadharisha kwamba ijapokuwa Umoja wa Afrika umefanikiwa kusuluhisha mizozo kadha iliozuka barani Afrika katika siku za karibuni, na mizozo michache imesalia inayotaka suluhu, hata hivyo bado kazi kubwa imeikabili Umoja wa Afrika kufanikiwa kuzuia na kusuluhisha migogoro yote iliolivaa bara la Afrika.