Skip to main content

Kikao cha 63 cha Baraza Kuu la UM chafunguliwa rasmi

Kikao cha 63 cha Baraza Kuu la UM chafunguliwa rasmi

Majadiliano ya jumla ya Baraza Kuu la UM, kwenye kikao cha wawakilishi wote yalianzishwa rasmi asubuhi ya leo ambapo viongozi wa kimataifa waliwasilisha hoja zao kadha wa kadha kuhusu utaratibu unaofaa kuzingatiwa kimataifa ili kukabiliana na matatizo ya ulimwengu kipamoja.

"Umahiri wa uongozi ndio wenye uwezo wa kuhishimu ahadi zinazotolewa kwa kuzitekeleza, kama inavyostahiki, licha ya kuwepo upinzani wa kisiasa na upungufu wa fedha. Uongozi ndio unaotuhamasisha kutuma wanajeshi wa kimataifa kulinda amani kwenye maeneo ya mbali yenye migogoro. Ni umahiri wa uongozi wenye uwezo wa kutetea hadharani haki.” Alisema KM uongozi unaoridhisha ndio wenye uwezo wa kuchukua hatua zinazofaa kukabiliana na matatizo yanayochochewa na mabadiliko ya hali ya hewa duniani, sera za kulinda viwanda vya nchini na kufanya makubaliano yenye natija kwa wote. Alisema mkusanyiko wa viongozi wa kimataifa hapa Makao Makuu, kwenye majadiliano ya wawakilishi wote, huupatia ulimwengu fursa kuu ya kuwa na matumaini mema, na kuondosha mashaka, kwa imani ya kwamba tukijumuika kipamoja, chini ya uongozi wa kimataifa, tutaweza kuyatekeleza mahitaji ya umma wa kimataifa kwa siku zijazo. Alikumbusha kwamba matatizo yaliokabili walimwengu ni matatizo yaliosababishwa na walimwengu wenyewe, na yatatatuliwa kwa mchango wa umma wa kimataifa na uongozi unaofaa."