Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale (Taarifa za Kusoma)

Hapa na Pale (Taarifa za Kusoma)

Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) limeripoti kwamba wiki iliopita watu 12,000 waliuhajiri mji wa Mogadishu, Usomali kwa sababu ya mapigano makali yaliozuka baina ya wapiganaji wafuasi wa makundi ya KiIslam, wenye kupinga serikali, dhidi ya na vikosi vya serikali vinavyoungwa mkono na majeshi ya Ethiopia yaliopo nchini. Nusu ya wahamiaji waliong’olewa makwao walipatiwa makazi ya muda karibu na mji, na nusu nyengine walikimbilia mji wa Afgooye ,uliopo kilomita 3o kusini-magharibi ya Mogadishu.

Serikali ya Kanada imeamua kuongeza, kwa mwezi mmoja zaidi, shughuli za manowari zake zinazolinda meli zenye kubeba shehena za misaada ya kiutu ambayo hufadhiliwa umma muhitaji katika Usomali na Shirika la UM juu ya Miradi ya Chakula Duniani (WFP). Meli kadha zilizokodiwa na WFP zinazochukua misaada ya chakula, katika siku za nyuma, zilikuwa zikitekwa nyara na maharamia, vitendo ambavyo vilihatarisha maisha ya karibu watu milioni tatu Usomali wenye kutegemea posho ya chakula wanayofadhiliwa na UM. Baadhi ya watu binafsi wenye kumiliki meli hizo, walitishia kufuta maafikiano ya kuhudumia WFP, kwa kuogopa vyombo vyao huenda vikatekwa nyara na maharamia, kitendo ambacho kingeliwanyima umma muhitaji tani 100,000 za chakula na kunusuru maisha. Manowari za Kanada zilikusudiwa kumaliza shughuli zao za kulinda meli zenye shehena ya misaada ya chakula ya WFP, katika mwambao wa Usomali, mnamo tarehe 27 Septemba, na Kanada SASA HIVI imeamua kuongeza muda wa shughuli hizo hadi tarehe 23 Oktoba 2008.

Tume ya Kupiga Vita Njaa kutoka Jamhuri ya Ireland imewasilisha ripoti maalumu kwenye Makao Makuu ya UM Alkhamisi, ikiwa miongoni mwa shughuli za mapitio ya utendaji wa Malengo ya Maendeleo ya Milenia. Ireland ilibuni Tume kwa makusudio ya kufafanua ni mchango wa aina gani unahitajika ujumuishwe nao kusaidia zile juhudi za kimataifa za kupunguza njaa duniani. Ripoti imetoa mapendekezo kwenye sehemu tatu muhimu: awali, ilitaka serikali ya Ireland iwasaidie kifedha wakulima wadogo wadogo Afrika kuongeza uzalishaji wa mavuno yao; pili, ilitakiwa kuimarisha juhudi za kupunguza na kudhibiti bora vifo vya uzazi na watoto wachanga na, tatu, kutekeleza ahadi za sasa za kimataifa, na pia kuhakikisha kuna mwambatano hakika kwenye juhudi za kimataifa za kukabiliana na tatizo la njaa katika mataifa yanayoendelea.

Kwenye mkutano wa mwaka wa Mradi wa Kimataifa wa Clinton (CGI) unaokutana New York hivi sasa, ilitangazwa rasmi kwamba Kampuni ya YUM! Brands itafadhilia Shirika la UM juu ya Miradi ya Chakula Duniani (WFP), dola milioni 80 za kuwasaidia watoto wa skuli wenye njaa, katika nchi zinazoendelea, kupata posho ya chakula kwa mwaka mzima wanaohudhuria masomo. Hii ni miongoni mwa hatua za pamoja za kukabiliana na lengo la awali la Maendeleo ya Milenia la kukomesha umaskini uliokithiri na kufyeka tatizo la njaa duniani. Kampuni ya YUM! Brands ni shirikisho la makampuni ya TACO Bell, Pizza Hut na Kentucky Fried Chicken ambayo huuza vyakula vya haraka vya kuondoka navyo. CGI ni mradi ulioanzishwa 2005 na Raisi Mstaafu wa Marekani Bill Clinton. WFP imeahidi kuwapatia chakula watoto milioni moja ziada katika kipindi kizima cha mwaka wa masomo, huduma ambayo itawasaidia watoto maskini katika nzhi kuendeleza masomo kwa afya itakayowapatia natija ya kimaisha kwa siku za mbele.