Skip to main content

Mapitio ya siku ya pili ya majadiliano ya jumla ya Baraza Kuu

Mapitio ya siku ya pili ya majadiliano ya jumla ya Baraza Kuu

Waziri Mkuu wa Uchina Wen Jiabao aliwaamabia wajumbe waliohudhuria kikao cha wawakilishi wote cha Baraza Kuu kwamba sera adhimu ya taifa lake ni kufuatilia njia ya amani kukuza maendeleo,wakati ikijenga nguvu za kijeshi kwa makusudio pekee ya kulinda na kuhami uhuru wake na umoja wa nchi. Alisema Uchina hauna dhamira yeyote ya “kumiliki dunia, si sasa wala si katika siku zijazo.”

José Ramón Machado Ventura, Naibu Raisi wa Kwanza wa Cuba alizungumza kwenye mjadala wa jumla katika Baraza Kuu kwa niaba ya Umoja wa Nchi Zisiofungamana Kisiasa Upande WoWote (NAM) ambapo alishtumu ya kuwa nchi maskini zinaendelea kuhimili madhara ya sera “ziliokosa mantiki, sera za ubadhirifu na za ulanguzi” zinazoendelezwa na baadhi ya mataifa tajiri, ambayo hutumia nguvu zao za kiuchumi na kiteknolojia, kwa njia zisio halali, kudumisha tofauti za fursa na utovu wa usawa miongoni mwa mataifa. Alikumbusha kwamba kutokana na sera kama hizo ndio maana pengo la kimaisha baina ya mataifa tajiri na mafukara linaendelea “kupanuka kila kukicha”. Alisema hata yale “Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs) ambayo ni ya wastani, na yenye kuwasilisha ndoto kwa asilimia kubwa ya umma wa nchi zinazoendelea, nayo pia yatashindwa kutekelezwa” na kuuvua umma husika na ufukara kwa sababu ya mfarakano huo unaohitajia kurekibishwa.

Raisi Shimon Peres wa Israel alisema kwenye hotuba yake,katika majadiliano ya Baraza Kuu,ya kuwa yeye binafsi anaamini mwelekeo wa mazungumzo ya hivi sasa kati yao na WaFalastina, yanaweza kukamilishwa katika kipindi cha mwaka mmoja, na kumalizika kwa kuwasilisha Mataifa mawili jirani ambayo raia zao wataishi kwa amani, usalama na katika hali ya kuhishimiana.

Raisi wa Senegal Abdoulaye Wade kwenye risala yake mbele ya kikao cha wawaklilishi wote alipendekeza wahisani wa kimataifa waekeze kwenye kilimo katika nchi zinazoendelea na kutumia utaratibu huo kukuza maendeleo badala ya kufadhilia misaada ya chakula, marekibisho ambayo, alitilia mkazo, yanahitajika kukabiliana na matatizo ya karne tuliomo hivi sasa. Alinasihi kwamba hatuwezi tena kutumia suluhu ya karne ya 20 kutatua matatizo magumu na ya pande nyingi ya karne ya 21 yanayoyakabili mataifa maskini.