Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

KM wa UM amesema, kwa kupitia msemaji wake, kwamba amehuzunishwa na kifo cha Raisi wa Zambia, Levy Patrick Mwanawasa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika . Aliitumia aila ya Raisi Mwanawasa na kwa umma wa Zambia mkono wake wa taazia katika kipindi hiki kigumu cha maombolezi.~

Wawakilishi wa Serikali ya Mpito Usomali pamoja na kundi la wapinzani la Umoja wa Ukombozi wa Pili wa Usomali, ambao walikutana Ijumatatu nchini Djibouti kwenye mkutano uliosimamiwa na Mjumbe Malumu wa KM kwa Usomali, Ahmedou Ould Abdallah walitiliana sahihi mapendekezo kadha ikijumlisha maafikiano ya kusitisha mkabiliano wa silaha baina yao, na pia kukubaliana kujizuia kutumia lugha ya uchokozi na uchochezi. Halkadhalika, makundihusika yaliafikiana kubuni mfumo maalumu wa kufuatilia utekelezaji wa mwafaka huu.

KM amemteua Peter Taksoe-Jensen wa Denmark kuwa KM Msaidizi juu ya Masuala ya Sheria, nafasi ambayo hapo kabla ilishikwa na Larry Johnson wa Marekani. Taksoe-Jensen alikuwa Waziri Mdogo wa Masuala ya Sheria na Mkuu wa Huduma za Sheria katika Wizara ya Mambo ya nje ya Denmark, na tangu 2004 alikuwa mshauri maalumu wa sheria ya kimataifa wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Denmark.

Wataalamu 2,000 ziada wanaohusika na taaluma ya maji, kutoka nchi kadha za dunia, wanakusanyika hivi sasa kwenye mji wa Stockholm, kuhudhuria kikao cha 18 cha mwaka cha 'Wiki ya Maji Safi Duniani'. Baadhi ya mashirika ya UM nayo pia yanahudhuria kikao cha Stockholm. Shirika la UM juu ya Makaazi (UN-HABITAT) limetoa ombi linayoyataka mataifa wanachama kujitahidi kuimarisha usafi duniani ili kuhakikisha itakapofika 2015 watu bilioni 1.5 walionyimwa huduma hizo watafadhiliwa mazingira safi ya kudhibiti afya.

Raisi wa Baraza la Usalama kwa mwezi Agosti, Balozi Jana Grauls wa Ubelgiji ametoa taarifa yenye kulaani vikali shambulio la bomu la kujitolea mhanga liliofanyika kwenye chuo cha polisi Algeria Ijumanne, na kuua darzeni za watu pamoja na kujeruhi kadhaa wengineo. Wajumbe wa Baraza walipeleka mkono wa taazia kwa waathiriwa wa kile walichokiita “kitendo cha kuchukiza cha kigaidi” na kusisitiza umuhimu wa kuwafikisha mahakamani wakosaji, wapangaji na wafadhili wa shambulio hilo haraka iwezekanavyo.