Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uamuzi wa ICC kuilazimisha UNAMID kuhamisha wafanyakazi Darfur

Uamuzi wa ICC kuilazimisha UNAMID kuhamisha wafanyakazi Darfur

UM inajiandaa hivi sasa kukabiliana na athari za uamuzi wa Luis Moreno-Ocampo, Mwendesha Mashitaka wa Mahakama ya Kimataifa Juu ya Jinai ya Halaiaki (ICC) ambaye alituma ombi rasmi kwa tume ya majaji watatu la kumshika Raisi Omar Hassan Ahmad AlBashir wa Sudan, aliyetuhumiwa kushiriki kwenye makosa ya vita na jinai dhidi ya utu pamoja na mauaji ya halaiki katika Darfur.

Mashirika yote mawili ya UM yenye kusimamia ulinzi wa amani kusini Sudan yaani UNMIS, na katika Darfur, kwa ushirikiano na Umoja wa Afrika, UNAMID, yameripoti hali kijumla nchini ni shwari. UNAMID imearifu doria za usalama pamoja na shughuli za kulinda misafara inayochukua misaada ya kihali na huduma nyenginezo za kiutu zote zinaendelezwa kama kawaida katika Darfur.

Wafanyakazi wanaohudumia misaada ya kiutu nao pia wanaendeleza operesheni zao za kugawa chakula kwa umma dhaifu, na kuwapatia maji safi na vifaa vya kimaisha umma muhitaji, na pia kuhudumia afya, hasa waathiriwa wa vitendo vya kunajisiwa kimabavu na kuwapatia hifadhi inayofaa raia husika.

Kuhusu operesheni za UM katika Khartoum, Shirika la UNMIS limeripoti kuendelea kuchangisha huduma zake muhimu za kusaidia wadau na washirika husika nchini Sudan kutekeleza, kwa wakati, mapendekezo ya Mapatano ya Jumla ya Amani yanayoambatana na hali kusini.

UNMIS imeripoti kufanyika maandamano matatu dhidi ya uamuzi wa Mwendesha Mashitaka wa ICC - maandamano yalifanyika katika miji ya Kassala, El Obeid na Khartoum na yote yalikuwa bila fujo. Maandamano ya Khartoum yalifanywa mbele ya ofisi ya UM ya UNDP. Hakuna maandamano yalioripotiwa kufanyika katika Darfur Ijumanne.

Serikali ya Sudan imeahidi kwa kauli nzito ya kwamba itaendelea kuwapatia watumishi wa UM wanaohusika na huduma za kiutu, pamoja na walinzi amani waliopo nchini hifadhi yote kinga dhidi ya fujo.