Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

KM Ban Ki-moon amesifu na kupongeza azimio liliopotishwa kwenye Mkutano wa kidiplomasiya uliofanyika Dublin, Ireland ambapo wajumbe wa Mataifa 111 waliridhia hati ya mkataba mpya wa kimataifa wa kupiga marufuku matumizi ya vile vibomu vya mtawanyo, na vile vile amehimiza Mataifa Wanachama kuidhinisha haraka mkataba na kuufanya chombo cha sheria ya kimataifa.

Agathon Rwasa, kiongozi wa kundi la waasi wa Palipehutu-FNL, aliripotiwa kurejea Burundi karibuni, hatua ambayo KM Ban aliiunga mkono kwa matumaini kwamba kitendo hicho kitahamasisha makundi yanayohasimiana kushirikiana kipamoja kurudisha utulivu na amani nchini na kukomesha mapigano yaliozuka karibuni kati ya Palipehutu-FNL na vikosi vya Serikali ya Burundi.

[na mwishowe] Wiki nne baada ya Kimbunga Nargis kugharikisha maeneo kadha wa kadha katika Myanmar UM umeanza kuona dalili za kutia moyo kuhusu huduma za dharura katika Myanmar baada ya Serikali kuamua kuruhusu watumishi zaidi wa kimataifa, wanaohudumia misaada ya kiutu, kuendeleza shughuli zao kwenye yale maeneo yalioharibiwa na kudhuriwa na tufani; na wakati huo huo UM imetoa mwito wenye kunasihi wenye madaraka Myanmar kutowalazimisha waathiriwa wa Kimbunga Nargis wa eneo la Delta ya Ayeyarwady, ambao hivi sasa wapo kwenye makazi ya muda, kurejea makwao bila ya idhini yao na kabla mastakimu hayajadhibitiwa, kijumla, kwa utaratibu utakaowawezesha kuanzisha maisha mapya bila ya matatizo.