Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ripoti ya 2008 juu ya Uchumi na Maendeleo Afrika yawasilishwa

Ripoti ya 2008 juu ya Uchumi na Maendeleo Afrika yawasilishwa

Wiki hii wataalamu wawili wa uchumi kutoka Idara ya UM juu ya Masuala ya Uchumi na Jamii (DESA) waliwasilisha mbele ya wanahabari wa kimataifa waliopo Makao Makuu, ripoti ya mwaka, iliotayarishwa bia na Kamisheni ya UM kuhusu Maendeleo ya Uchumi Afrika (ECA) pamoja na Umoja wa Afrika. Mada ya ripoti ilikuwa na kichwa cha maneno kisemacho \'Ripoti ya Uchumi Maendeleo kwa Afrika.\'

Wataalamu wachumi wa DESA walifahamisha ya kuwa sehemu ya kwanza ya ripoti ya ECA na Umoja wa Afrika ilielezea zaidi mwelekeo wa maendeleo ya uchumi na matumaini yaliotarajiwa katika 2008; na sehemu ya pili ilizingatia maendeleo ya jamii na ukuaji wa uchumi katika 2007 na kuashiria matarajio kwa 2008. Kozul-Wright alitanabahisha ya kuwa tafiti zao hasa zilijaribu kukadiria hali ya uchumi ilivyo sasa hivi Afrika, kwa kuambatana na yale mapendekezo ya kufufua uchumi wa bara hilo, yaliopitishwa kwenye Mkutano wa Kimataifa juu ya Ugharimiaji wa Huduma za Maendeleo, uliofanyika 2002 kwenye mji wa Monterrey, Mexico.

Mchumi wa pili, Hong alibainisha sababu zilizosaidia uchumi wa Afrika kukua kwa nguvu ya kiasi katika miaka ya karibuni, hali ambayo alisema chanzo chake kilitokana na kukithiri kwa mahitaji ya bidhaa asilia, kijumla, katika ulimwengu, na vile vile kwa sababu ya kuongezeka kwa bei za bidhaa katika soko za kimataifa. Hata hivyo, aliendelea kusema Hong, shughuli za maendeleo ya uchumi barani Afrika hazikulingana wala kufanyika kwa usawa; kwa mfano, maeneo ya Afrika ya Mashariki yaliongoza katika kuendeleza uchumi uliokua kwa nguvu, na wakati huo huo zile sehemu za Afrika ya Kati zilionyesha kupwelewa kimaendeleo.

Lakini licha ya hayo yote, ripoti imebashiria 2008 utakuwa ni mwaka wenye matarajio ya kutia moyo Afrika, kimaendeleo, pindi utulivu utaendelea katika sekta fulani fulani za uchumi – mathalan, ikiwa mahitaji ya bidhaa asilia katika mataifa yenye utamaduni wa viwandani yataendelea kuwa ya nguvu, na bei zitaendelewa kuwa katika kiwango cha juu. Hali hiyo ikijiri maendeleo ya Afrika yatazidi kunyanyuka.

Lakini ripoti vile vile ilikumbusha kwamba ni idadi ndogo ya nchi za Afrika ambazo hivi sasa zinafaidika na kuwemo kwenye ule mkondo sahihi wa kuyafikia baadhi ya yale Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs) kwa wakati. Kwa sababu tafiti za kimataifa zimethibitisha kwamba miongoni mwa mataifa 50 ziada barani Afrika chini ya nchi 20 tu zinakadiriwa kuweza kuyatekeleza Malengo ya Milenia, kwa wastani. Hata hivyo, ripoti ilimaliza kwa sauti ya kutia moyo kwa kusema kwamba uamuzi wa kuanzishwa kwa tume maalumu itakayojumuisha wahisani wa kimataifa wenyedhamira ya kuyasaidia mataifa ya Afrika kiuchumi, pamoja na ile rai ya kufanyisha Mkutano wa kila mwaka wa Mawaziri wa Afrika kufuatilia maendeleo kijumla katika utekelezaji wa mapendekezo ya Monterrey, hatua hizi ni za ujasiri mkubwa utakaosaidia kusukuma mbele maendeleo Afrika kwa kasi inayoridhisha na yenye natija kwa wote.