Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mtaalamu wa UM anahadharisha, uzalishaji wa nishati kwa nafaka hufukuta mzozo wa chakula duniani

Mtaalamu wa UM anahadharisha, uzalishaji wa nishati kwa nafaka hufukuta mzozo wa chakula duniani

Ijumatatu, Jean Ziegler, Mkariri Maalumu wa Ofisi ya UM juu ya Haki za Binadamu anayehusika na haki ya watu kupata chakula, alikuwa na mahojiano ya mwisho na waandishi habari kabla ya kukamilisha muda wa kazi na taasisi hiyo ya kimataifa.

Ziegler alishtumu kwamba makampuni makuu ya kimataifa yanayohusika na biashara ya nafaka ndio yenye kusababisha mifumko mikubwa ya bei ya chakula duniani. Vile vile aliilaumu Marekani kwa kuamua kuunguza fungu kubwa la akiba yake ya nafaka kutengenezea nishati. Alionya Ziegler kwamba thuluthi moja ya umma wote wa kimataifa, ilio sawa na watu bilioni 2.2 bado huishi kwenye mazingira ya ufukara uliohanikiza, hali ambayo, alitilia mkazo huwanyima fungu hili la wanadamu, mahitaji yao ya kimsingi ya kila siku, na anakhofia bei ya chakula ikiendelea kupanda umma husiku utashindwa kumudu chakula kwa muda mrefu kabiisa.

Ziegler alijaribu kuihamasisha jamii ya kimataifa kudhibiti mgogoro wa mifumko ya bei ya chakula katika soko la kimataifa, haraka iwezekanavyo, kabla mzoo huo haujazusha maafa mapya ya njaa pamoja na machafuko, hali ambayo anaashiria kusababisha idadi kubwa ya vifo, hasa katika nchi zinazoendelea.