Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Juhudi za kufufua hadhi ya kazi za taasisi ya Baraza Kuu katika UM.

Juhudi za kufufua hadhi ya kazi za taasisi ya Baraza Kuu katika UM.

Raisi wa Baraza Kuu Srgjan Kerim alipokutana na waandishi habari wa kimataifa, hapa Makao Makuu, wiki hii, kuzingatia kikao cha mwaka cha 62, alibainisha matukio ya kutia moyo.

Alisema tangu mwezi Septemba, pale alipoanza kuongoza mijadala ya wawakilishi wote katika Baraza Kuu, alishuhudia mwelekeo wa maana katika juhudi za Mataifa Wanachama kufufua tena hadhi halali ya taasisi hii ya kimataifa, juu ya namna inahudumia majukumu muhimu kadha wa kadha iliyodhaminiwa nayo na Mkataba wa UM, licha ya kuwa maamuzi ya Baraza la Usalama ndiyo yenye madaraka ya kulazimisha mapendekezo yake kuwa ni sheria ya kimataifa, wakati maazimio ya Baraza Kuu mara nyingi hutafsiriwa kuwa ni mapendekezo ya kutekelezwa kwa hiyari tu. Hata hivyo, Raisi KERIM alikumbusha kwamba asilimia kubwa ya masuala muhimu yanayoambatana na taratibu za kuimarisha maisha bora ya umma wa kimataifa, mathalan udhibiti bora wa athari za mabadiliko ya hali ya hewa, taratibu za kufadhilia maendeleo ya kiuchumi na jamii, na hata namna ya kusimamia mageuzi kwenye kazi za UM, haya ni masuala ambayo hujadiliwa kidhati, sio katika Baraza la Usalama, bali katika Baraza Kuu la UM, ambapo ndipo penye jukwaa linalowakilisha umma wote wa dunia, na kwenye mastakimu yenye uwezo wa kuleta maaafikiano na suluhu ya kuridhisha kimataifa.

Kadhalika, Raisi wa Baraza Kuu, Srgjan Kerim alisisitiza kwenye mazungumzo yake na waandishi habari ya kuwa hakuna haja, hivi sasa, ya kupitisha azimio la kuidhinisha ufufuaji wa kazi za Baraza Kuu, kwa sababu azimio kama hilo “halihitajiki tena”, hususan tukizingatia namna Mataifa Wanachama yalivyopania kwenye kikao cha mwaka huu katika kukuza ushirikiano wa hadhi ya juu baina yao, na kushadidia umuhimu wa kuyatatua masuala yanayosumbua walimwengu kipamoja. Alisema mijadala yenye mada kiini, kama ule mjadala uliofanyika kwenye Baraza Kuu kuzingatia kipamoja suala la ugaidi, hatua hiyo inaaminika itasaidia pakubwa kuongoza mjadala wa mapitio ulioandaliwa kufanyika mwezi Septemba mwakani utakaosailia Mradi wa Kimataifa Kupiga Vita Ugaidi Duniani.