Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wawakilishi wa KM wakutana na Raisi Kabila kusailia usalama katika Kivu

Wawakilishi wa KM wakutana na Raisi Kabila kusailia usalama katika Kivu

Mnamo mwanzo wa wiki, Mwakilishi Maalumu wa KM katika Jamhuri ya Kideomkrasi ya Kongo (DRC), William Swing akifuatana na Kamanda Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi wa Amani vya UM vya MONUC, Jenerali Boubacar Gueye Walikutana kwa mashauriano na Raisi Joseph Kabila kwenye mji wa Goma, kaskazini-mashariki ya nchi, kusailia hali ya usalama katika jimbo la Kivu Kaskazini, eneo ambalo karibuni lilizongwa na hali ya mapigano baina ya vikosi vya Serikali na wanajeshi waasi walio’ongozwa na Jenerali Mtoro Laurent Nkunda.

Mkutano huu ulihudhuriwa vile vile na Mabalozi wa Afrika Kusini, Marekani, Ubelgiji, Ufaransa, na pia Uingereza. Baada ya mkutano kulitolewa taarifa rasmi ya pamoja iliosisitiza kwamba wanajeshi waasi wanawajibika kujiunga haraka, na bila masharti, na Jeshi la Taifa. Msemaji wa KM Michele Montas alitangaza wanajeshi waasi 363, wafuasi wa Jenerali Mtoro Nkunda wameshajisalimisha na sasa wanajiandaa kujiunga na Jeshi la Taifa. Halkadhalika, Shirika la Ulinzi wa Amani katika JKK (MONUC) limeripoti kuwa litaendelea kuimarisha mchango wake kuhudumia vikosi vya Jeshi la Taifa na kuisaidia Serikali ya JKK kurudisha utulivu na amani katika maeneo yote ya utawala nchini kama ilivyoidhinishwa na Baraza la Usalama.