Hapa na pale

Hapa na pale

Tarehe 16 Oktoba huadhimishwa na Shirika la UM juu ya Chakula na Kilimo (FAO) pamoja na aila nzima ya UM kuwa ni ‘Siku ya Chakula kwa Wote Duniani’. Siku hii hutumiwa kuwazindua walimwengu ya kwamba watu milioni 854 bado wanaendelea kuteswa na kusumbuliwa, kila siku, na tatizo sugu la njaa na ukosefu wa chakula, idadi ya waathiriwa ambayo inazidi kukithiri kwa sababu ya mifumo dhaifu ya kilimo, ugawaji usiotosheleza wa chakula, uwezo usiofaa wa kuhifadhia chakula, na vile vile kutokana na hali ya vurugu na mapigano, mazingira ambayo hukwamisha huduma za kilimo kwenye maeneo husika.

Tarehe 17 Oktoba iliadhimishwa na mamilioni ya umma wa kimataifa, katika sehemu mbalimbali za dunia, kuwa ni ‘Siku ya Kutetea Ukomeshaji wa Umasikini Duniani.’

Baraza Kuu la UM wiki hii limefanyisha mjadala maalumu wa wawakilishi wote kuzingatia suala la Ushirikiano Mpya wa Maendeleo katika Afrika (NEPAD) kwa lengo la kuimarisha amani, kustawisha uchumi maendeleo na kudhibiti hali ya vurugu na mapigano barani humo.

[na hatimaye] KM ameripoti kwa Baraza la Usalama kwamba ameamua kuwateua Wawakilishi Maalumu watatu kwa Liberia, JKK na Cote d’Ivoire: Ellen Margrethe Loj wa Denmark anatarjiwa kupelekwa Liberia; Alan Doss wa Uingereza kupelekwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na kuchukua nafasi ya William Swing, aliye Mjumbe Maalumu wa KM hivi sasa; na Choi Young-Jin wa Jamhuri ya Korea ameteuliwa kumwakilisha KM katika Coote d'Ivoire. Kadhalika KM ameliarifu Baraza la Usalama kwamba kuwa amewateua Bibi Bintou Keita wa Guinea kuwa Naibu Mjumbe Maalumu kwa Burundi na Bacre Waly Ndiaye wa Senegal kuwa Naibu KM Maalumu kwa JKK.