Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Juhudi za kuisaidia Uganda kukabiliana na mafuriko.

Juhudi za kuisaidia Uganda kukabiliana na mafuriko.

Ofisi ya UM inayohusika na Misaada ya Dharura, au Ofisi ya OCHA, imeripoti kwamba eneo la Uganda mashariki limekabwa na mafuriko makubwa baada ya mvua kali kunyesha katika mwisho wa Julai.

Kwa mujibu wa OCHA, watu 2,000 katika wilaya za Katakwi na Amura walilazimika kuhama makazi, na nyumba 4,000 zilisharipotiwa kupoteza akiba yao yote ya mavuno kutokana na mafuriko. Kadhalika, Shirika la Msalaba Mwekundu Uganda limethibitisha watu 50,000 katika wilaya za Amuria na Katakwi, na pia katika maeneo ya Budada, Bukeda, Kumi na Sironko, Uganda mashariki, wameathirika vibaya sana kihali kutokana na uharibifu uliochohewa na mafuriko. Halkadhalika, mafuriko yameharibu mabarabara na madaraja, hali ambayo imekwamisha zile juhudi za mashirika ya kimataifa za kupeleka misaada ya dharura ya kihali na kiutu kwenye maeneo muhitaji. Ofisi ya OCHA imeonya ikiwa mzozo huu hautodhibitiwa mapema, kuna hatari ya kufumka kwa kasi maradhi ya kuambukiza, kama vile malaria, ugonjwa wa kuharisha pamoja na magonjwa ya ngozi, na vile vile kuzusha matatizo ya minyoo ya matumboni, maradhi ya pumu na ugonjwa wa kifua.

Timu ya wataalamu wa UM na Serekali ya Uganda inatazamiwa kuanzisha shughuli zake kwenye majimbo ya Teso na Mbale mwisho wa wiki, ambapo itajaribu kutathminia mahitaji ya umma katika huduma za usafi, maji ya matumizi, hali ya afya, akiba ya chakula, hifadhi ya makazi na hali za mabarabara. Wataalamu hawa wanawakilisha mashirika ya UM ya chakula na kilimo (FAO), maendeleo ya watoto (UNICEF), miradi ya chakula (WFP) na pia kutoka Ofisi ya OCHA, na vile vile kutakuwepo na wawakilishi wa Shirika la Msalaba Mwekundu la Uganda na kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu.