Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Makundi ya wanamgambo 3,500 katika Ituri kukubali kusalimisha silaha

Makundi ya wanamgambo 3,500 katika Ituri kukubali kusalimisha silaha

Makundi matatu ya wanamgambo wa JKK katika wilaya ya Ituri, yaani Mouvement Revolutionnaire Congolais (MRC), Front de Résistance Patriotique de l’Ituri (FRPI) na Front des Nationalistes et Intégraionnistes (FNI) yameahidi kusajili jumla ya wapiganaji wao 3,500 kwenye ule mpango wa UNDP ujulikanao kama mradi wa DDR, mpango ambao utawawezesha wanamgambo husika kupatiwa msaada wa fedha za kuanzisha maisha mapya ya kiraia au kujiunga na jeshi la taifa.

UNDP inakadiria asilimia 70 ya wapiganaji wa zamani watajiunga na jamii za kiraia, wakati asilimia 30 iliobakia itaamua kujiunga na jeshi la taifa.

Wanamgambo walioridhia maisha ya kiraia watafadhiliwa msaada wa dola 110, posho ambayo wanatarajiwa kuitumia kulipa gharama za usafiri, na pia kulipia ushuru wa kadi ya ajira inayohitajika kwenye zile shughuli za ajira ya kufufua huduma za uchumi maendeleo, mathalan, katika shughuli za ujenzi wa mabarabara, utengenezaji wa maskuli yalioharibiwa wakati wa mapigano, na pia kuimarisha miradi ya afya na mazingira safi. Kila mtu atakayeshiriki kwenye kadhia hizi atalipwa dola 2 kwa siku kwa muda wa siku 90. Kadhalika, pindi wanamgambo hawa wa zamani wataamua kuanzisha biashara, wameahidiwa kufadhiliwa mikopo khafifu na mashirika ya kizalendo yasio ya kiserekali.

Mjumbe Maalumu wa KM kwa DRC na aliye mkuu wa Shirika la MONUC, William Swing, akifuatana na Kamanda Mkuu wa vikosi vya UM, Jenerali Babacar Gaye, walizuru kwa siku mbili mji wa Ituri katika Bunia, kutathminia maendeleo ya mradi wa DDR. Wakuu hawa wa UM walitilia mkazo kwenye risala zao juu ya umuhimu wa kuhakikisha washirikishwa wote wanaosalimisha silaha kutekeleza kidhati mapendekezo yote ya mradi wa DDR kama inavyopaswa kisheria.