Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yaonya, 'muongezeko wa uhamiaji duniani wahatarisha usalama wa afya kijumla'

WHO yaonya, 'muongezeko wa uhamiaji duniani wahatarisha usalama wa afya kijumla'

Shirika la Afya Duniani (WHO) Alkhamisi limewasilisha Ripoti juu ya Hali ya Afya Ulimwenguni kwa 2007. Ripoti iliwasilishwa mjini Geneva na imeonya kwamba muongezeko wa uhamaji mkubwa kati ya mataifa ya dunia, na vile vile kukithiri kwa fungamano za uhusiano miongoni mwa mataifa, ni hali iliyozusha mfumko mkubwa, na wa kasi, wa maradhi ya kuambukiza ulimwenguni. Kwa mujibu wa WHO mazingira haya yanahatarisha, kwa ujumla, usalama wa afya ya umma ulimwenguni.

Ripoti ya WHO ilisisitiza ya kuwa tatizo hili la afya halitoweza kudhibitiwa kama inavyotakikana bila ya kuimarisha ushirikiano wa karibu sana miongoni nchi wanachama. Kati ya mapendekezo yaliotiliwa mkazo na ripoti kuzingatiwa ni pamoja na umuhimu wa Mataifa yote Wanachama kutekeleza kwa ukamilifu, na kwa dharura, yale Maafikiano ya 2005 juu ya Kanuni za Kuongoza Afya ya Kimataifa.