Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uchambuzi wa NGOs kuhusu mijadala ya Tume ya UM juu ya Haki za Wenyeji wa Asili Duniani

Uchambuzi wa NGOs kuhusu mijadala ya Tume ya UM juu ya Haki za Wenyeji wa Asili Duniani

Wasikilizaji, mnamo mwezi Mei, kwa muda wa wiki mbili mfululizo, wawakilishi wa jamii za wenyeji wa asili kutoka pembe mbalimbali za ulimwengu walikutana kwenye Makao Makuu ya UM na kuhudhuria Kikao cha Sita cha Tume ya Kudumu ya UM juu ya Masuala yanayohusu Haki za Wenyeji wa Asili Duniani.

UM imekadiria idadi ya jamii za wenyeji wa asili katika dunia inafika watu milioni 370. Kikao cha mwaka huu kilisisitiza umma huu ni lazima upatiwe fursa ya kushirikishwa kwenye mijadala inayozingatia taratibu za kuleta suluhu ya ile migogoro inayohusu haki ya kumiliki ardhi na mali ya asili iliopo kwenye maeneo ya wenyeji wa asili, na vile vile kuhakikisha kuwa wanapatiwa taarifa na ripoti kamili kuhusu masuala haya kwa lugha ambayo wanaifahamu na kuielewa. Mapendekezo mengineyo yaliopitishwa kwenye kikao cha mwaka huu ni pamoja na kuihimiza jumuiya ya kimataifa kuwafadhilia wenyeji wa asili misaada ya fedha, na pia ufundi, unaohitajika kukamilisha ramani ya vipimo vya mipaka ya maeneo yao, na kuhakikisha kuwepo sheria ya kitaifa inayotoa adhabu kwa wale wanaoendeleza vitendo haribifu kwenye ardhi ya wenyeji wa asili, na kuzilipa jamii hizo fidia kutokana na vitimbi vinavyokiuka haki zao.

Makala hii imejumuisha mahojiano na Helen Nkoyo, mwanaharakati wa Kenya anayehusika na hekaheka za kuwasaidia wenyeji wa asili kupigania haki zao kitaifa. Kadhalika tulifanya mahojiano na Mary Simat, anayewakilisha shirika lisio la kiserekali linalogombania haki za wanawake Afrika pamoja na Profesa Elijah K. Biamah wa Kitivo cha Uhandisi cha Chuo Kikuu cha Nairobi.

Sikiliza mahojiano haya kwenye redio ya mtandao.