Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Matumizi kwa ajili ya silaha yapunguzwe na hatua zichukuliwe kuokoa SDGs: UN

Nembo za SDG katika Ukumbi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (kutoka Maktaba)
UN Photo/Manuel Elías
Nembo za SDG katika Ukumbi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (kutoka Maktaba)

Matumizi kwa ajili ya silaha yapunguzwe na hatua zichukuliwe kuokoa SDGs: UN

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J. Mohammed leo amewataka viongozi wa kimataifa kuelekeza rasilimali kutoka kwenye vita kwenda kwenye mipango ya amani na maendeleo endelevu.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu Stenhouse Umoja Stenhouse Mataifa António Guterres, kwenye jukwaa la ngazi ya juu la kisiasa la Umoja wa Mataifa kuhusu malengo ya mmaendeleo endelevu HLPF, ngazi ya mawaziri Bi. Mohamed ametoa wito wa kuchukuliwa hatua za haraka na madhubuti ili kuokoa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) yanayolegalega hivi sasa.

"Migogoro huko Gaza, Sudan, Ukraine, na kwingineko inasababisha hasara kubwa ya maisha na kugeuza umakini wa kisiasa na rasilimali chache kutoka kwenye kazi ya haraka ya kutokomeza umaskini na kuepusha janga la mabadiliko ya tabianchi,"

Amesisitiza haja ya kupunguza bajeti za kijeshi na badala yake kuelekeza fedha hizo katika kudumisha amani na maendeleo.

Hatua muhimu katika SDGs

Akiangazia hali mbaya ya SDGs, Bibi Mohammed amebainisha kuwa ni asilimia 17 tu ya malengo hayo ndio yako kwenye mstitari wakati ukomo wa utimizaji wa malengo hayo mwaka 2030 unakaribia.

Naibu Katibu Mkuu amesisitiza kkuwa "Vizazi vijavyo vinastahili zaidi ya asilimia 17 ya mustakabali endelevu," akielezea mkakati wa pande nne wa kuongeza kasi ya haraka katika jitihada za kufikia tarehe ya mwisho ya 2030 ya Malengo hayo.

Amesema hatua ya kwanza ni kudumisha amani, akisisitiza kwamba rasilimali za kisiasa na kifedha zinapaswa kuelekezwa kutoka kweye migogoro hadi kwenye juhudi za maendeleo.

Pia amesisitiza umuhimu wa mabadiliko yanayojali mazingira na ya kidijitali, akiyahimiza mataifa kuboresha mipango yao ya utekelezaji wa mabadiliko ya tabianchi ifikapo mwaka 2025, kuyapatanisha na kikomo cha nyuzi joto 1.5 kulingana na Mkataba wa Paris na kuwekeza katika kupanua wigo wa uunganishwaji kidijitali.

Naibu Katibu Mkuu wa UN Amina Mohammed  akihutubia jukwaa la ngazi ya juu la kisiasa la Umoja wa Mataifa HLPF2024
UN Photo/Loey Felipe
Naibu Katibu Mkuu wa UN Amina Mohammed akihutubia jukwaa la ngazi ya juu la kisiasa la Umoja wa Mataifa HLPF2024

Kuwekeza katika amani

Akizungumzia changamoto za kifedha zinazokwamisha maendeleo ya SDG, Bi. Mohammed ametaja pengo linaloongezeka la ufadhili na kuzorotesha hali ya kifedha katika nchi nyingi zinazoendelea.

Ametambua mageuzi yanayoendelea ya benki za maendeleo za kimataifa na urejelezaji wa haki maalum za uchoraji lakini ametaka hatua madhubuti zaidi zichukuliwe.

"Lazima twende mbele zaidi na haraka ili kutoa kichocheo cha SDG," alihimiza, akitoa wito wa kuongezeka kwa uwezo wa kukopesha, kupanua wigo wa ufikiaji wa ufadhili wa dharura, na suluhisho kamili la madeni.

Kutimiza ahadi

Kwa kumalizia, Bi. Mohammed amesisitiza ahadi ya SDGs ya "kutomwacha mtu nyuma".

Akihimiza haja ya kuwapa kipaumbele watu walio katika mazingira magumu, kuzingatia haki za watu wenye ulemavu na kupambana na ukosefu wa usawa wa kijinsia.

Amesema "Kufikia ajenda hii kunamaanisha kuwaweka watu walio katika mazingira magumu na makundi hatarishi katika mstari wa mbele kwenye mipango ya maendeleo ya taifa, sera na bajeti".

Rais wa Baraza Kuu Dennis Francis, akihutubia mkutano wa mawaziri  wakati wa HLPF 2024
UN Photo/Manuel Elías
Rais wa Baraza Kuu Dennis Francis, akihutubia mkutano wa mawaziri wakati wa HLPF 2024

Mataifa lazima yachukue hatua

Rais wa Baraza Kuu Dennis Francis ameunga mkono udharura hii, akiangazia masaibu ya watu bilioni 1.1 wanaoishi katika umaskini wa kila aina.

"Leo, watu bilioni 1.1 wanaishi katika umaskini wa aina mbalimbali. Ikiwa hatutafanya chochote chenye athari, asilimia nane ya idadi ya watu duniani au watu milioni 680 bado watakuwa na njaa ifikapo 2030," ameonya, akitaka hatua za haraka na za kinazichukuliwe.

Amesisitiza haja ya kushughulikia sababu za msingi za umaskini na njaa, akisisitiza kuunganishwa kwake na migogoro, mabadiliko ya tabianchi, na majanga ya kiuchumi.

Kuwa wabunifu na jasiri

Bwana Francis pia amesisitiza umuhimu wa Mkutano wa SDG wa mwaka jana, ambao ulipitisha tamko kali la kisiasa na kuzindua awamu mpya ya hatua za kasi ili kufikia malengo ya maendeleo ya kimataifa ifikapo mwaka 2030.

Akiwa na matarajio, ameonyesha matumaini kwa Mkutano ujao wa kilele wa “Wakati Ujao”, unaotazamiwa kuwa tukio la mageuzi ambalo litaimarisha utashi wa kisiasa na kushughulikia pengo la ukosefu wa usawa wa mfumo wa kifedha wa kimataifa.

"Matokeo yanayotarajiwa ya mkutano huo, Mkataba wa Wakati Ujao lazima yawe mageuzi ya kutosha ili kupigia kengele kwa haki dhamira ya kisiasa ambayo italeta mustakbali angavu kwa wote, kila mahali," amesema, akizitaka nchi wanachama kuwa wabunifu, kuwa na umoja na ujasiri, kuhakikisha. Mkataba huo ni wa mabadiliko ya kweli na unarejesha imani ya umma.

Paula Narváez Ojeda Rais wa ECOSOC akizungumza wakati wa mkutano wa  ngazi ya mawaziri  kwenye HLPF 2024
UN Photo/Manuel Elías
Paula Narváez Ojeda Rais wa ECOSOC akizungumza wakati wa mkutano wa ngazi ya mawaziri kwenye HLPF 2024

Kusaidia kutimiza Malengo

Naye Paula Narvaez, Rais wa Baraza la Kiuchumi na Kijamii la  Umoja wa Mataifa ECOSOC, amesisitiza jukumu muhimu la chombo hicho katika kusimamia utekelezaji wa SDGs.

"Katika mzunguko wa Baraza la Kiuchumi na Kijamii, nimeweka kipaumbele kukuza sera za mageuzi ambazo mashirika tanzu mbalimbali ya Baraza yanaweza kutoa kutekeleza SDGs."

Amesisitiza umuhimu wa kurekebisha sera hizi ili kukidhi mahitaji mbalimbali ya watu na sayari huku akizingatia matatizo ya kila nchi.

Katika muktadha huo, ameangazia mapitio muhimu ya kitaifa ya hiyari yaliyofanywa katika HLPF, na nchi 36 ziliwasilisha mwaka huu. Mapitio haya yanatoa taswira muhimu katika uzoefu wa kitaifa, mafunzo tuliyojifunza, na vikwazo vilivyojitokeza katika kutekeleza SDGs.

"Tumeweza kuchunguza kwa kina zaidi sababu za kucheleweshwa kwa utekelezaji, lakini pia tumeweza kusikia kutoka kwa serikali wenyewe na pande zinazohusika kuhusu mazoea mazuri ambayo tunaweza kuzalisha," amebainisha Bi. Narváez.

Kikao cha mawaziri

Wakati wa kikao cha siku tatu cha mawaziri, HLPF itafanya mjadala wa jumla kuhusu mada Kuanzia Mkutano wa SDG hadi Mkutano wa Wakati Ujao.

Mawaziri na wawakilishi wa ngazi za juu wa nchi zinazoshiriki, pamoja na mashirika ya serikali, makundi makubwa na washikadau wengine watachukua hatua ili kutimiza Azimio la Kisiasa la Mkutano wa Kilele wa SDG wa 2023 na kuharakisha utekelezaji wa Ajenda ya 2030 ya Maendeleo Endelevu na SDGs.

Pia watachangia matayarisho ya Mkutano wa Kilele wa Wakati Ujao, utakaofanyika Septemba mwaka huu.

Likifanyika chini ya mwamvuli wa ECOSOC, Jukwaa hilo la HLPF litahitimishwa tarehe 18 Julai kwa kupitishwa kwa tamko la mawaziri.