Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mbinu gani zinahitajika kutokomeza njaa na umasikini ifikapo 2030? - HLPF2024

Rais wa  Baraza la Kiuchumi na Kijamii la Umoja wa Mataifa ECOSOC Paula Narváez  akizungumza katika Jukwaa la ngazi ya juu la Kisiasa la Umoja wa Mataifa HLPF2024 kuhusu malengo ya Maendeleo endelevu
UN Photo/Loey Felipe
Rais wa Baraza la Kiuchumi na Kijamii la Umoja wa Mataifa ECOSOC Paula Narváez akizungumza katika Jukwaa la ngazi ya juu la Kisiasa la Umoja wa Mataifa HLPF2024 kuhusu malengo ya Maendeleo endelevu

Mbinu gani zinahitajika kutokomeza njaa na umasikini ifikapo 2030? - HLPF2024

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Jukwaa la kisiasa la ngazi ya juu la Umoja wa Mataifa HLPF kuhusu malengo ya maendeleo endelevu SDGs limeendelea leo kweye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani huku wadau kutoka nchi mbalimbali wanachama wakijikita na melengo mawili ya maendeleo endelevu SDGs.

Malengo yaliyomulikwa leo ni SDG1 ambalo ni kutokomeza umasikini na SDG2 la kutokomeza njaa ifikapo mwaka 20230.

Kutokomeza umasikini

Katika jukwaa hilo kuhusu lengo la kwanza la kutokomeza umasikini SDG 1 na maingiliano wake na malengo mengine ya maendelea washiriki wameangazia  Je, ni sera gani madhubuti, jumuishi na ubia na hatua pana zaidi, zilizolengwa zinaweza kuharakisha mafanikio ya SDG 1?

Pia wametathimini ukuaji wa polepole wa uchumi unaathiri vipi utekelezaji wa SDG 1?

Zaidi ya hapo washiriki wa jukwaa hilo wamejadili pia jinsi gani uhusiano na Malengo mengine ya maendeleo unaweza kufikiwa kikamilifu ili kuhakikisha sera bora zaidi na shirikishi za kutokomeza umaskini katika aina na vipimo vyake vyote. Ili kusaidia kutimiza lengo la SDG1.

Lengo la SDG2 la kutokomeza njaa
United Nations
Lengo la SDG2 la kutokomeza njaa

Kutokomeza njaa

Lengo la pili la kutokomeza njaa SDG2 ni moja ya malengo yenye changamoto kubwa kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa hata kutokana na hali ya dunia  ilivyo kwa sasa ikighubikwa na vita karibu kila kona, majanga ya asili na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Katika juhudi za kuhakikisha lengo hilo linafikiwa ifikapo mwaka 2030 wajumbe wametathimini uhusiano uliopo baina ya SDG2 na malengo mengine ya maendeleo.

Lakini pia wameangalia Je, migogoro ya kimataifa inaathiri vipi uhakika wa chakula na lishe duniani?

Wameenda mbali zaidi na kujadili je, tunawezaje kuharakisha vitendo na kuimarisha ushirikiano ili kukomesha njaa na utapiamlo na kutambua haki ya chakula cha kutosha kwa kila mtu?

Pia katika kupata suluhu wamejadaili Je, ni suluhu zipi za kibunifu na mbinu bora za kilimo endelevu na zenye mnepo zinaweza kuwa jawabu na ni zipi?

Na mwisho kabisa wanetathimini kuhusu, ushirikiano wa kimataifa na kikanda kwenye mifumo ya chakula unachangia vipi katika kusongesha utemizaji wa SDG 2?

Naibu Katibu Mkuu wa UN Amina Mohammed  akihutubia jukwaa la ngazi ya juu la kisiasa la Umoja wa Mataifa HLPF2024
UN Photo/Loey Felipe
Naibu Katibu Mkuu wa UN Amina Mohammed akihutubia jukwaa la ngazi ya juu la kisiasa la Umoja wa Mataifa HLPF2024

Wito wa kuchukua hatua za kuleta mabadiliko

Mkutano huo ulioanza Julai 8 utakabilika Julai 18 na akizungumza katika ufunguzi Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J. Mohammed alitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuwa “ni lazima iitimize haraka ahadi na uwekezaji unaohitajika ili kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ifikapo tarehe ya mwisho ya mwaka  2030.”

Bi. Mohammed alitoa wito wa kuwepo kwa mageuzi na sera shupavu ili kukabiliana na changamoto za kimataifa kama vile umaskini, uhaba wa chakula na mabadiliko ya tabianchi.

"Ingawa changamoto kubwa zilizo mbele yetu ni za kutisha, kwa pamoja tunaweza kuzishinda, kufikia mustakabali wenye amani, ustawi na endelevu ambao watu wote sio tu wanauhitaji bali wanastahili," aliwaambia wajumbe waliokusanyika kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, jijini New York.

Watoto kutoka mji wa Xochimilco wakiwa wamebeba mabango ya malengo ya maendeleo endelevu SDGs
UNIC Mexico/Antonio Nieto
Watoto kutoka mji wa Xochimilco wakiwa wamebeba mabango ya malengo ya maendeleo endelevu SDGs

HPLF 2024

Chini ya mwamvuli wa Baraza la Kiuchumi na Kijamii la Umoja wa Mataifa ECOSOC, mada ya mwaka huu inalenga katika kutokomeza umaskini kwa njia endelevu, suluhu za kiubunifu huku kukiwa na migogoro mingi.

Hadi tarehe 17 Julai, Jukwaa litatathimini maendeleo kuelekea Lengo la 1 la kutokomeza umaskini, Lengo la 2 la kutokomeza njaa, Lengo la 13 kuhusu hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, Lengo la 16 la jamii zenye amani na ushirikishwaji, na Lengo la 17 la kuimarisha njia za utekelezaji wa malengo hayo.

Kwenye kalenda ya jukwaa hilo pia kuna tathimini za hiyari za Kitaifa (VNR), ambapo nchi huripoti kwa hiari maendeleo yao kuelekea ufikiaji wa SDGs, changamoto zinazowakabili na mipango yao ya kuzishinda. Mikutano kadhaa ya kandoni itafanyika na maonyesho pia yamepangwa mwishoni mwa HLPF.