Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatimaye Julai 7 yatambuliwa na Baraza Kuu la UN kuwa Siku ya Kimataifa ya Kiswahili

Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Hussein Kattanga akiwasilisha rasimu ya azimio la kuitambua tarehe 7 Julai kila mwaka kuwa Siku ya Kimataifa ya lugha ya Kiswahili.
United Nations
Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Hussein Kattanga akiwasilisha rasimu ya azimio la kuitambua tarehe 7 Julai kila mwaka kuwa Siku ya Kimataifa ya lugha ya Kiswahili.

Hatimaye Julai 7 yatambuliwa na Baraza Kuu la UN kuwa Siku ya Kimataifa ya Kiswahili

Utamaduni na Elimu

Hauchi hauchi umekucha, hayawi hayawi yamekuwa, hakika asiye na mwana aeleke jiwe, hatimaye leo Julai Mosi, Azimio (A/78/L.83) la kutaka Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liitambue Julai 7 kuwa Siku ya Kimataifa ya Kiswahili limepitishwa bila kupingwa.

Uamuzi huu uliokuwa unasubiriwa kwa hamu na wadau wa lugha hii ya Kiswahili kote duniani, umefanyika kuanzia saa 9 za alasiri kwa saa za New York katika ukumbi wa Baraza Kuu kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa nchini Marekani.

Rasimu ya Azimio hilo imepitia mchakato mrefu chini ya uratibu wa ‘nchi za Kiswahili’ kama vile Kenya, Tanzania na Burundi kwa kusaidiwa na UNESCO, Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni ambalo tangu tarehe 23 Novemba 2021 tayari lilishaitambua Julai 7 kuwa Siku ya Kimataifa ya Lugha ya Kiswahili.

Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa Balozi Hussein A. Kattanga, kwa niaba ya nchi za Muungano wa Afrika amepewa nafasi ya kuwasilisha ombi mbele ya Baraza.

Kwa hatua hii ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kukubali kila Julai 7 yawe maadhimisho ya Kimataifa ya lugha ya Kiswahili, inategemewa kuitangaza zaidi lugha hii ya kwanza kwa kuwa na wazungumzaji wengi zaidi kwenye nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara na ambayo ni ya 10 duniani kwa kuzungumzwa na watu wengi zaidi, kwa mujibu wa UNESCO.

Tweet URL

Azimio lililopitishwa lilikuwa linasema kwamba:

Kwa kukumbuka azimio la Baraza la Umoja wa Mataifa namba 76/268 la tarehe 10 Juni 2022 kuhusu lugha mbalimbali, ambapo lilimhimiza Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuimarisha uungaji mkono wa lugha zisizo rasmi zinazozungumzwa duniani kote, kwa njia isiyo na gharama, kwa lengo la kufahamisha na kukuza ufahamu kuhusu historia, utamaduni na matumizi ya lugha hizo,

Kwa kurejelea azimio namba 41C/53 lililopitishwa na Mkutano Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO tarehe 23 Novemba 2021, ambapo lilitangaza tarehe 7 Julai ya kila mwaka kuwa Siku ya Lugha ya Kiswahili Duniani,

Kwa kuzingatia kuwa Kiswahili ni miongoni mwa lugha 10 zinazozungumzwa na watu wengi zaidi duniani, ikiwa na wazungumzaji zaidi ya milioni 200, ikiwa ni lugha katika nchi nyingi za Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika pamoja na Mashariki ya Kati, na kutambua jukumu la lugha hiyo katika kukuza amani, umoja na tofauti za kitamaduni, kujenga ufahamu na kukuza mijadala miongoni mwa watu,

Kwa kuzingatia kuidhinishwa na kupitishwa kwa Kiswahili kama lugha rasmi na ya kazi ya Muungano wa Afrika, Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika, SADC na Jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC kama nyenzo muhimu katika kukuza utangamano wa kikanda,

Kwa kutambua umuhimu wa kuongeza ufahamu wa maadili mbalimbali ya kiuchumi na kiutamaduni ya lugha ya Kiswahili na mchango wake kama kichocheo cha amani, umoja na maendeleo ya kijamii na kiuchumi, kwa nia ya kutekeleza Ajenda ya 2030 ya Maendeleo Endelevu,

Baraza likaamua:

  1. Kutangaza tarehe 7 Julai ya kila mwaka kuwa Siku ya Lugha ya Kiswahili Duniani, itakayoadhimishwa kila mwaka kuanzia 2024;
  2. Linaalika Nchi zote Wanachama, mashirika na wadau wa mfumo wa Umoja wa Mataifa, mashirika mengine ya kimataifa na kikanda na wadau wengine husika, zikiwemo asasi za kiraia, mashirika yasiyo ya kiserikali, taasisi za kitaaluma, sekta binafsi na watu binafsi, kuiona Siku ya Lugha ya Kiswahili Duniani kuwa inafaa, ili kuongeza ufahamu wa historia, utamaduni na matumizi ya lugha;
  3. Baraza linaalika Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO na Idara ya Mawasiliano ya Kimataifa ya Sekretarieti ya Umoja wa Matafa, DGC kuwezesha maadhimisho ya Siku ya Lugha ya Kiswahili Duniani, kwa kushirikiana na mashirika mengine husika ya mfumo wa Umoja wa Mataifa, kwa kuzingatia masharti kiambatisho cha azimio la Baraza la Uchumi na Kijamii, ECOSOC, 1980/67;
  4. Linasisitiza kuwa gharama za shughuli zote zinazoweza kutokea kutokana na utekelezaji wa azimio hili zinapaswa kufikiwa kwa michango ya hiari, ikiwa ni pamoja na kutoka sekta binafsi, na kuwaalika wadau wote husika kuchangia na kuunga mkono maadhimisho ya Siku ya Lugha ya Kiswahili Duniani;
  5. Linamsihi Katibu Mkuu azimio kwa Nchi zote Wanachama, mashirika ya mfumo wa Umoja wa Mataifa na wadau wengine husika, zikiwemo asasi za kiraia, sekta binafsi na wasomi kwa uzingatiaji unaofaa.
Siku ya lugha ya Kiswahili duniani
UN News
Siku ya lugha ya Kiswahili duniani