Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Huu ni ushindi mkubwa kwa lugha ya Kiswahili – Mabalozi Burundi, Kenya na Tanzania

Mahojiano na Balozi Njambi Kinyungu(kushoto), Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Kenya, Balozi Zephyryin Maniratanga, Mwakilishi wa Kudumu wa Burundi(Kati) na Balozi Hussein Kattanga(kulia), Mwakilishi wa kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa kuhusu Siku…
UN News
Mahojiano na Balozi Njambi Kinyungu(kushoto), Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Kenya, Balozi Zephyryin Maniratanga, Mwakilishi wa Kudumu wa Burundi(Kati) na Balozi Hussein Kattanga(kulia), Mwakilishi wa kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa kuhusu Siku ya Kimataifa ya Kiswahili jijini New York Marekani.

Huu ni ushindi mkubwa kwa lugha ya Kiswahili – Mabalozi Burundi, Kenya na Tanzania

Utamaduni na Elimu

Bara la Afrika lina nchi 54 katika ya nchi 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa lakini katika lugha 6 rasmi za Umoja wa Mataifa, hakuna hata lugha moja ya kiafrika na huo pamoja na sababu nyingine ndio umekuwa msukumo wa kundi la Afrika katika Umoja wa Mataifa kupigania lugha ya Kiswahili itambulike katika Umoja wa Mataifa angalau kwa kuanza na siku maalumu kwa ajili ya lugha hii.

 

Ndipo Julai mosi, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa likapitisha kwamba kila mwaka tarehe 7 mwezi Julai itakuwa ni Siku ya Kimataifa ya Lugha ya Kiswahili.
 
Mara baada ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kufanya uamuzi huo, baadhi ya mabalozi wanaoziwakilisha ncho za Afrika katika Umoja wa Mataifa wakaketi na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa kueleza furaha yao kupitia mahojiano yaliyofanywa na na Anold Kayanda.
 
Balozi Njambi Kinyungu(kushoto), Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Kenya, Balozi Zephyryin Maniratanga(kulia), Mwakilishi wa Kudumu wa Burundi katika Umoja wa Mataifa wakizungumza na Anold Kayanda wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Ma…
UN News
Balozi Njambi Kinyungu(kushoto), Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Kenya, Balozi Zephyryin Maniratanga(kulia), Mwakilishi wa Kudumu wa Burundi katika Umoja wa Mataifa wakizungumza na Anold Kayanda wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani.
Balozi Zephyryin Maniratanga, Mwakilishi wa Kudumu wa Burundi katika Umoja wa Mataifa anasema, “tunaamini hatua hii ni ufunguo wa fursa nyingine nyingi kwa siku za usoni.”
 
Kwa Balozi Hussein Kattanga, Mwakilishi wa kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, ni imani yake kwamba ipo siku lugha ya Kiswahili itakuwa miongoni mwa lugha rasmi za Umoja wa Mataifa.
 
Matumaini yake hayo yameimarika zaidi baada ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Julai Mosi kuidhinisha lugha hii ya Kiswahili iwe na siku maalumu ya kuiadhimisha kila mwaka. Tarehe 7 Julai Siku ya Kimataifa ya Lugha ya Kiswahili.
Kwa upande wake Balozi Njambi Kinyungu, Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Kenya katika Umoja wa Mataifa, anaona fursa kubwa mbele baada ya hatua hii ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuipatia hadhi kubwa lugha ya Kiswahili kiasi kwamba sasa imeingia katika Siku za Umoja wa Mataifa.
 
“Lugha ya Kiswahili ina faida nyingi kwa Umoja wa Mataifa na pia sisi nchi ambazo tunaongea Kiswahili,” anasema Balozi Kinyungu akiongeza kwamba, “Kiswahili ni ajira. Wale ambao wamesoma Kiswahili, wale ambao wana fundisha Kiswahili. Pia Kiswahili ni huduma.”
 

Azimio lililopitishwa lilikuwa linasema kwamba:

 
Kwa kukumbuka azimio la Baraza la Umoja wa Mataifa namba 76/268 la tarehe 10 Juni 2022 kuhusu lugha mbalimbali, ambapo lilimhimiza Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuimarisha uungaji mkono wa lugha zisizo rasmi zinazozungumzwa duniani kote, kwa njia isiyo na gharama, kwa lengo la kufahamisha na kukuza ufahamu kuhusu historia, utamaduni na matumizi ya lugha hizo,
 
Kwa kurejelea azimio namba 41C/53 lililopitishwa na Mkutano Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO tarehe 23 Novemba 2021, ambapo lilitangaza tarehe 7 Julai ya kila mwaka kuwa Siku ya Lugha ya Kiswahili Duniani,
 
Kwa kuzingatia kuwa Kiswahili ni miongoni mwa lugha 10 zinazozungumzwa na watu wengi zaidi duniani, ikiwa na wazungumzaji zaidi ya milioni 200, ikiwa ni lugha katika nchi nyingi za Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika pamoja na Mashariki ya Kati, na kutambua jukumu la lugha hiyo katika kukuza amani, umoja na tofauti za kitamaduni, kujenga ufahamu na kukuza mijadala miongoni mwa watu,
 
Kwa kuzingatia kuidhinishwa na kupitishwa kwa Kiswahili kama lugha rasmi na ya kazi ya Muungano wa Afrika, Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika, SADC na Jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC kama nyenzo muhimu katika kukuza utangamano wa kikanda,
 
Kwa kutambua umuhimu wa kuongeza ufahamu wa maadili mbalimbali ya kiuchumi na kiutamaduni ya lugha ya Kiswahili na mchango wake kama kichocheo cha amani, umoja na maendeleo ya kijamii na kiuchumi, kwa nia ya kutekeleza Ajenda ya 2030 ya Maendeleo Endelevu,
 
Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Hussein Kattanga akiwasilisha rasimu ya azimio la kuitambua tarehe 7 Julai kila mwaka kuwa Siku ya Kimataifa ya lugha ya Kiswahili.
United Nations
Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Hussein Kattanga akiwasilisha rasimu ya azimio la kuitambua tarehe 7 Julai kila mwaka kuwa Siku ya Kimataifa ya lugha ya Kiswahili.

Baraza linaamua:

 
Kutangaza tarehe 7 Julai ya kila mwaka kuwa Siku ya Lugha ya Kiswahili Duniani, itakayoadhimishwa kila mwaka kuanzia 2024;
 
Linaalika Nchi zote Wanachama, mashirika na wadau wa mfumo wa Umoja wa Mataifa, mashirika mengine ya kimataifa na kikanda na wadau wengine husika, zikiwemo asasi za kiraia, mashirika yasiyo ya kiserikali, taasisi za kitaaluma, sekta binafsi na watu binafsi, kuiona Siku ya Lugha ya Kiswahili Duniani kuwa inafaa, ili kuongeza ufahamu wa historia, utamaduni na matumizi ya lugha;
 
Baraza linaalika Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO na Idara ya Mawasiliano ya Kimataifa ya Sekretarieti ya Umoja wa Matafa, DGC kuwezesha maadhimisho ya Siku ya Lugha ya Kiswahili Duniani, kwa kushirikiana na mashirika mengine husika ya mfumo wa Umoja wa Mataifa, kwa kuzingatia masharti kiambatisho cha azimio la Baraza la Uchumi na Kijamii, ECOSOC, 1980/67.
 
Linasisitiza kuwa gharama za shughuli zote zinazoweza kutokea kutokana na utekelezaji wa azimio hili zinapaswa kufikiwa kwa michango ya hiari, ikiwa ni pamoja na kutoka sekta binafsi, na kuwaalika wadau wote husika kuchangia na kuunga mkono maadhimisho ya Siku ya Lugha ya Kiswahili Duniani;
 
Linamsihi Katibu Mkuu azimio kwa Nchi zote Wanachama, mashirika ya mfumo wa Umoja wa Mataifa na wadau wengine husika, zikiwemo asasi za kiraia, sekta binafsi na wasomi kwa uzingatiaji unaofaa.