Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkulima Zambia: Tumegeukia mazao ya chakula kulinda afya badala ya tumbaku

Mkulima Zambia: Tumegeukia mazao ya chakula kulinda afya badala ya tumbaku

Pakua

Nchini Zambia, mpango wa shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ulimwenguni, WHO, Kanda ya Afrika wa kuhamasisha wakulima kuachana na kilimo cha tumbaku na badala yake kulima mazao mbadala umeanza kuzaa matunda kama anavyoelezea mmoja wa wakulima walioitikia wito huo.

Tuko wilaya ya Chipangali nchini Zambia ambako video ya WHO kanda ya Afrika inaanzia katikati ya shamba lililostawi la mahindi na mtu mmoja akitembea katikati na kisha anajitokeza akiwa na tabasamu! Huyu ni Titus Mwanza, mkulima wa zamani wa tumbaku ambaye amekipa kisogo kilimo hicho na kugeukia mazao mengine. Kulikoni?

“Niliacha kulima tumbaku miaka minne iliyopita Kilichonifanya niache kulima zao hili ni matatizo yaliyokuweko kwenye familia yangu, na faida haikuwa nzuri. Vile vile ugonjwa wa saratani au kansa unaohusishwa na zao hili. Wale wanaovuta wanapata aina mbali mbali za magonjwa.”

Uelewa huu unafuatia ziara ya mwishoni mwa mwaka 2022, ambapo Bwana Mwanza na wakulima wenzake wawili kutoka Zambia walishiriki ziara ya mafunzo nchini Kenya ambako mashamba ya kwanza kabisa yasiyo na tumbaku yalianzishwa mwaka 2021. Katika mashamba hayo wakulima 6,000 wa tumbaku tayari wameacha kulima zao hili na wanalima mazao mbadala.

Baada ya kurejea Zambia anasema,

“Niliacha kilimo cha tumbaku na kuanza kulima mazao mengine. Mazao kama maharage ya soya, alizeti, karanga na maharage. Hayo ndio mazao ninayolima kwa sasa.”

Bwana Mwanza amekuwa mkulima kiongozi akifundisha wenzake kilimo mbadala na tayari amefundisha wakulima 50.

“Kinachotuhamasisha ni kwamba tunalima kile ambacho baadaye tunakula. Tunalima mahindi, kisha tunakula. Tunalima mbaazi, kisha tunakula. Tunatengeneza maziwa kutokana na maharage ya soya. Vile vile tunatumia maharage ya soya kutengeneza soseji. Ni kitu ambacho tunalima na kisha tunakula. Ni chakula chenyewe. Tumbaku sio chakula, tumbaku ni dawa.”

Video inatamatika huku Bwana Mwanza akiwa kwenye shamba lake la mahindi lililostawi vizuri, mahindi yamekomaa na tabasamu kamili usoni mwake.

Audio Credit
Cecily Kariuku
Sauti
2'7"
Photo Credit
© UNICEF/Karin Schermbrucker