Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tahadhari mpya ya njaa yatolewa Gaza ambapo familia hukaa siku nzima bila chakula

Mwanamke anapika mkate ndani ya jiko la kupikia lililojengwa na matope katika Ukanda wa Gaza.
© UNRWA
Mwanamke anapika mkate ndani ya jiko la kupikia lililojengwa na matope katika Ukanda wa Gaza.

Tahadhari mpya ya njaa yatolewa Gaza ambapo familia hukaa siku nzima bila chakula

Amani na Usalama

Gaza bado iko kwenye tahadhari ya njaa baada ya wataalam wa uhakika wa chakula kuonya hii leo kwamba zaidi ya kaya moja kati ya tano "hukaa siku nzima bila kula".

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo vya vyombo vya habari na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula duniani WFP kutoka Roma nchini Italia, ripoti ya Mfumo Unganishi wa Uainishaji wa Uhakika wa Chakula (IPC) kuhusu Gaza inatoa taswira kamili ya njaa inayoendelea, ikigundua kuwa asilimia 96 ya watu amabao ni saw ana watu milioni 2.15 wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula katika kiwango cha shida au zaidi (IPC daraja la 3+), na karibu watu laki tano wakiwa katika kiwango cha daraja la 5.

Ripoti hii mpya imeonesha kuimarika kidogo ikilinganishwa na tathmini ya awali ya mwezi Machi, ambayo ilionya kuhusu uwezekano wa njaa katika maeneo ya kaskazini mwa Gaza mwishoni mwa Mei.

Hata hivyo ripoti hiyo ya IPC imebainisha kuwa ilimradi machafuko yanaendelea katika eneo zima la Ukanda wa Gaza basi hatari kubwa ya njaa itaendelea kuwepo kutokana na upatikanaji wa misaada ya kibinadamu kuendelea kuzuiliwa.

Uboreshaji huo umetokana na kuongezeka kwa usambazaji wa chakula kaskazini mwa Gaza pamoja na huduma za lishe ambazo zimesaidia kupunguza viwango vya njaa, ijapokuwa bado watu wapo katika hali ya kukata tamaa.

WFP pia ina wasiwasi mkubwa kutokana na uwezo kupungua sana wa mashirika ya kibinadamu kutoa msaada muhimu huko kusini mwa Gaza na wanasema hii itahatarisha maendeleo yaliyopatikana. Mapigano huko Rafah mwezi Mei yaliwafanya zaidi ya watu milioni moja kuyahama makazi yao na kupunguza kwa kiasi kikubwa ufikishaji wa misaada ya kibinadamu.

Wakati huo huo, ombwe la usalama limekuza uvunjaji wa sheria na machafuko ambayo yanatatiza sana shughuli za kibinadamu. WFP sasa inahofia kwamba eneo la kusini mwa Gaza hivi karibuni linaweza kuona viwango sawa vya njaa vilivyorekodiwa hapo awali katika maeneo ya kaskazini mwa Gaza.

Watu wakitafuta maji katika mji wa Khan Younis kusini mwa Ukanda wa Gaza.
© UNICEF/Eyad El Baba
Watu wakitafuta maji katika mji wa Khan Younis kusini mwa Ukanda wa Gaza.

Hakuna hata sentimita moja iliyo salama

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva Uswisi baada ya kutumwa kwa mara ya pili huko Gaza, Yasmina Guerda kutoka ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya Kibinadamu OCHA amesema Hakuna "sentimita salama zilizosalia" huko Gaza ambapo sheria za vita zinaendelea kupuuzwa kwa gharama ya watu wa eneo lililoharibiwa na mashirika ya kibinadamu.

Guerda amewaeleza waandishi wa habari kuwa utoaji wa misaada umekuwa "kitendawili cha kila siku" ambacho kimewaacha watoto wenye utapiamlo bila msaada wa kuokoa maisha wanaohitaji.

“Uchunguzi wa moja kwa moja niliofanya nikiwa huko kila siku ni kwamba hakuna sentimita salama iliyobaki Gaza. Hakuna mahali unaweza kuwa na uhakika kwamba hakutakuwa na shambulio usiku huo, “alisema.

Baada ya takriban miezi tisa ya mashambulizi makali ya Israel na mashambulizi ya ardhini yaliyochochewa na mashambulizi ya kigaidi yanayoongozwa na Hamas na utekaji nyara tarehe 7 Oktoba, mahitaji ya kimsingi ni makubwa kuliko wakati mwingine wowote kwa wananchi wa Gaza waliolazimika kuyakimbia makazi yao kulingana na maagizo ya mara kwa mara ya kuwataja kuhama yanayotolewa na jeshi la Israel.

“Mtu unapewa dakika 10 hadi 15 kuondoka kwenye jengo lako kwa sababu litapigwa kwa bomu. Watoto wako wanalala katika chumba jirani,” Bi Guerda alisema.

Aliongeza kuwa “Lazima ufanye maamuzi ndani ya sekunde ili kuamua ni nini cha kufunga, ni nini muhimu na unafafanuaje kile ambacho ni muhimu? Vyeti vya kuzaliwa, vitambulisho, fomula ya watoto… Ni hadithi niliyoisikia mara kutoka kwa watu waliokimbia Mji wa Gaza, Jabalia, Khan Younis, Deir Al-Balah na sasa bila shaka Rafah.”

Kutoa misaada ya kibinadamu kwa manusura hao na zaidi ya watu milioni moja walioondolewa kutoka Rafah kusini mwa Gaza katika muda wa siku 10 hadi 14 - bado ni vigumu sana, hasa tangu operesheni ya kijeshi ya Israel ilipofunga mpaka muhimu wa kuvuka huko mapema Mei, ofisa huyo wa OCHA alieleza.

Msichana mwenye umri wa miaka 11 ameketi kwenye vifusi vya nyumba huko Rafah, kusini mwa Ukanda wa Gaza.
© UNICEF/Eyad El Baba
Msichana mwenye umri wa miaka 11 ameketi kwenye vifusi vya nyumba huko Rafah, kusini mwa Ukanda wa Gaza.

Watoto wanazidi kuuawa

Naye Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA, Philippe Lazzarini, hakuna kupungua kwa gharama mbaya ya kibinadamu ya vita huko Gaza ambapo watoto 10 hupoteza mguu mmoja au yote kila siku, huku kukiwa na mashambulizi ya Israeli na hofu ya njaa.

“Kimsingi, kila siku tuna watoto 10 ambao wanapoteza mguu mmoja au miguu miwili kwa wastani. Hii inakupa wazo la upeo wa aina ya utoto, mtoto anaweza kuwa nayo Gaza,” alisema mkuu huyo wa UNRWA.

Katika taarifa yake kuhusu hali ya ukanda huo, Lazarrini alibainisha kuwa takriban watoto 4,000 wameripotiwa kutoweka na 17,000 hawana wasindikizaji baada ya karibu miezi tisa ya mgogoro mkali.

“Ongeza idadi hiyo kwa watoto 14,000 walioripotiwa kuuawa tangu mwanzo wa vita." Aliongeza Lazarrini kabla ya kulaani shambulio la hivi karibuni lililoripotiwa dhidi ya shule inayoendeshwa na shirika hilo katika mji wa Gaza.

“Hapo jana usiku, tena, shule imeshambuliwa katika eneo la kambi iliyoko ufukweni (Shati), ambayo iko kaskazini mwa Gaza. Na inasemekana tumesikia kuhusu watu 12 waliouawa, 22 wakijeruhiwa,” Mkuu huyo wa UNRWA aliwaambia waandishi wa habari.

Mkuu huyo wa UNRWA pia alisisitiza juu ya haja ya uwajibikaji kwa mashambulizi dhidi ya vituo vya Umoja wa Mataifa na wafanyakazi wote wa kibinadamu, ambayo yanakiuka sheria za kimataifa za kibinadamu.