Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ulimwengu unashindwa kushughulikia changamoto ya hali ya kupoteza kumbukumbu au Dementia 

Dementia ni moja ya sababu kuu za ulemavu na utegemevu miongoni mwa wazee kote ulimwenguni.
WHO/Cathy Greenblat
Dementia ni moja ya sababu kuu za ulemavu na utegemevu miongoni mwa wazee kote ulimwenguni.

Ulimwengu unashindwa kushughulikia changamoto ya hali ya kupoteza kumbukumbu au Dementia 

Afya

Ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Ulimwenguni, WHO iliyotolewa hii leo mjini Geneva, Uswisi yenye jina 'Hali ya ulimwengu kuhusu hatua za afya ya umma dhidi ya tatizo la kusahau',  inasema ni robo tu ya nchi zote ulimwenguni ambazo zina sera, mkakati au mpango wa kitaifa wa kusaidia watu walio na ugonjwa wa shida ya akili unaosababisha kupoteza kumbukumbu na hali nyingine kama kushindwa kufikiria vizuri.

Ripoti hiyo kifafanua zaidi imeeleza kuwa nusu ya nchi hizi ziko katika Kanda ya Ulaya ya WHO, na sehemu iliyobaki imegawanyika kati ya maeneo mengine ya ulimwengu. Wakati huo huo barani Ulaya mipango mingi iliyokuwepo kushughulikia tatizo hili la kupoteza kumbukumbu au dementia, imekwisha muda wake na hivyo ikionesha hitaji la serikali kujitolea upya kuweka mipango madhubuti ya kupambana na hali hii.  

Mkurugenzi wa WHO, Dkt Tedros Adhanom Ghebreyesus, amenukuliwa akisema, "ugonjwa wa kusahau unawaibia mamilioni ya watu kumbukumbu zao, uhuru na utu, lakini pia unatuibia sisi watu tunaowajua na tunaowapenda. Ulimwengu unawaangusha watu walio na shida ya akili, na hiyo inatuumiza sisi sote. Miaka minne iliyopita, serikali zilikubaliana malengo ya wazi ya kuboresha huduma za dementia. Lakini malengo pekee hayatoshi. Tunahitaji hatua za pamoja ili kuhakikisha kuwa watu wote walio na shida ya akili na kupoteza kumbukumbu wanaishi na msaada na hadhi inayostahili.” 

Aidha, WHO inaeleza kuwa idadi ya watu wanaoishi na ugonjwa wa shida ya akili na hivyo kupoteza kumbukumbu na uwezo wa kufikiri, inaongezeka ikikadiriwa kuwa zaidi ya watu milioni 55, ikiwa asilimia 8.1 ya wanawake na 5.4% ya wanaume wenye zaidi ya umri wa miaka 65 wanaishi na shida ya dementia. Idadi hii inakadiriwa kuongezeka watu milioni 139 ifikapo mwaka 2050. 

Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa na WHO, Ugonjwa wa kusahau husababishwa na magonjwa tofautitofauti na majeraha ambayo huathiri ubongo, kama ugonjwa wa Alzheimers au hata kiharusi. Ugonjwa huu unathiri kumbukumbu na kazi nyingine za utambuzi, pamoja na uwezo wa kufanya kazi za kila siku.