Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COVID-19 yatishia uwepo wa vyombo vya Habari- Guterres

Mwanahabari wa Redio Miraya Sudan Kusini akizungumza na mtoto
UNMISS/Isaac Billy
Mwanahabari wa Redio Miraya Sudan Kusini akizungumza na mtoto

COVID-19 yatishia uwepo wa vyombo vya Habari- Guterres

Utamaduni na Elimu

Kuporomoka kwa uwezo wa fedha kwa mashirika mengi ya umma ya vyombo vya habari duniani kote ni moja ya athari mbaya zaidi za janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres hii leo katka tukio lililofanyika na kuungwa mkono na Umoja wa Mataifa kwa lengo la kupigia chepuo sekta hiyo kuelea siku ya uhuru wa vyombo vya Habari duniani tarehe 3 mwezi ujao wa Mei.

Magazeti peke yake yakipoteza takribani dola bilioni 30 mwaka jana, "baadhi ya watu wanahofia kuwa janga la Corona linaweza kuwa tukio la kutowesha vyombo vya yhabari" ameonya Katibu Mkuu.

"Hatuwezi kuruhusu hilo litokee", amesema Guterres katika ujumbe wake kwa njia ya video kwenye tukio hilo. "Kuendeleza uandishi wa habari huru, unaozingatia taarifa sahihi ni huduma muhimu ya umma na ya msingi katika kujenga jamii salama, yenye afya na mustakabali usioharibu mazingira."

Tishio la ongezeko la Habari zisizo sahihi

Katibu Mkuu ametoa wito kwa nchi kusaidia Mfuko Mpya wa Vyombo Vya Habari vyenye maslahi ya umma, hususan kukwamua mustakabali wa mashirika huru ya vyombo vya habari katika nchi za kipato cha chini na kati.

Mjadala wa leo uliofanyika kuelekea siku ya Uhuru wa vyombo vya Habari duniani tarehe 3 mwezi ujao wa Mei, uliandaliwa kwa Pamoja na Idara ya Mawasiliano kwa Umma ya Umoja wa Mataifa, DGC kwa ushirikiano na shirika la kutoa misaada Luminate wakiunga mkono kampeni ya Verified, ambayo ni kampeni iliyoanzishwa na Umoja wa Mataifa kusambaza Habari za ukweli kuhusu COVID-19 . 

Picha ya makataba ikiwaonesha wanahabari wakipiga picha za video katika Makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani.
UN Photo/Ariana Lindquist
Picha ya makataba ikiwaonesha wanahabari wakipiga picha za video katika Makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani.

Janga la Corona limefichua jinsi upataji wa taarifa za uhakika ni zaidi ya suala la haki za binadamu, lakini pia in suala la uhai na kifo. Umoja wa Mataifa umekuwa ukifanya kazi kukabili usambazaji wa habari potofu na ufichaji wa habari sahihi sambamba na kauli za chuki, vitu ambavyo vimeongezeka kadri idadi ya wagonjwa wa COVID-19 inavyoongezeka.

Waziri wa Habari wa Ghana, Kojo Oppong-Nkrumah, akizungumza kwenye mkutano huo amsema ‘janga la habari, limeongeza mkwamo wa uchumi ambao tayari sekta ya habari ilikuwa inakabiliwa nayo.

"Kadri watu wanavyozidi kutengeneza taarifa za uongo na kuzisambaza, ndivyo mapato ya vyombo vya habari yanapungua vivyo hivyo viwango vya ueledi vinavyohitajika vinapata shida. Madhara yake ya jumla ni kwamba kuna tishio la watu kuamini vyombo vya Habari, hususan pale vinapoza kurusha mara kwa mara hizi habari zisizo na ukweli", amesema. 

Wanahabari wakikusanya taarifa katika moja ya matukio huko Moldova, Ulaya Mashariki
© UNICEF Moldova
Wanahabari wakikusanya taarifa katika moja ya matukio huko Moldova, Ulaya Mashariki

Kupunguzwa kwa mishahara, kupunguza watumishi na athari kwa afya ya akili

Janga la Corona ‘limenyonga’ sekta ya habari duniani kwa kuwa katika kipindi hicho, waandishi wa habari 14,000 pamoja na wasimamizi kwenye sekta hiyo walipunguzwa kazini katika nchi 125. Hiyo ni kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na kituo cha kimataifa cha wanahabari, ICJF kwa ushirikiano na Chuo Kikuu cha Columbia, vyote vyenye makao yake makuu nchini Marekani.

Vyombo vya habari vinategemea matangazo kupata mapato yake na zaidi ya asilimia 40 ya vyombo vya Habari viliripoti kushuka kwa matangazo kwa kati ya asilimia 50 hadi 75. Matokeo yake ni kukatwa kwa mishahara na wafanyakazi kupunguzwa, "katika kipindi ambacho watu walihitaji zaidi taarifa", amesema Joyce Barnathan, Rais wa ICFJ.

Taswira hiyo inaonesha athari ya afya ya akili kwa watu ambao wana jukumu la kuandaa na kusambaza Habari kuhusu COVID-19.

Takribani asilimia 70 ya waandishi wa habari walibaini kuwa athari za kisaikolojia na kihisia zilikuwa jambo gumu zaidi katika kazi zao. Theluthi moja ya idadi hiyo ilisema kuwa mashirika yao hayakuwapatia vifaa vya kujikinga. Utafiti mwingine wa kando umebaini kuwa wanawake waandishi wa Habari walikumbwa na mashambulizi wakifanya kazi zao hizo.

Demokrasia hatarini

Kadri chumi zinavyojikwamua taratibu kuelekea hali mpya ya sasa, Bi. Barnathan anatarajia mapato nayo kurejea. Hata hivyo amesema, anashangaa iwapo kiwango chake kitatosheleza kufadhili maslahi ya umma katika vyombo vya habari duniani kote kwa sababu kuna jambo liko hatarini.

"Kilicho hatarini siyo uandishi wa Habari bali, kwa maoni yangu, ni mustakabali wa demokrasia"’ amesema Rais huyo wa ICJF.

Kuvurugwa kwa ubunifu

Mfumo wa sasa wa utendaji wa uandishi wa Habari duniani kote umekufa, na matangazo yanasambazwa kupitia Facebook na njia nyinginezo, hivyo mshiriki mwingine, Maria Ressa kutoka Ufilipino ambaye ameshinda tuzo ya mwaka huu ya UNESCO amesisitiza kuwa mashirika ya vyombo vya Habari ya maslahi ya umma ni lazima yajihusishe na teknolojia ili yaweze kusalia imara.