Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maria Ressa wa Ufilipino kupokea tuzo ya UNESCO ya Guillermo 2021

Picha kutoka kwenye video wakati Maria Ressa alipokuwa akishiriki mkutano wa UNESCO kuhusu uhuru wa vyombio vya habari. (Mei 4, 2020)
UNESCO
Picha kutoka kwenye video wakati Maria Ressa alipokuwa akishiriki mkutano wa UNESCO kuhusu uhuru wa vyombio vya habari. (Mei 4, 2020)

Maria Ressa wa Ufilipino kupokea tuzo ya UNESCO ya Guillermo 2021

Haki za binadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) limemtaja mwandishi wa habari za uchunguzi na mkuu wa vyombo vya habari Maria Ressa wa Ufilipino kuwa ndio mtunukiwa wa tuzo yake ya uhuru wa vyombo vya habari kwa mwaka 2021. 

Kwa zaidi ya miongo mitatu, Bi. Ressa amehusika katika mipango mingi ya kukuza uhuru wa vyombo vya habari na kwa sasa anaendesha blog mashuhuri ijulikanayo kama Rappler.  

Kazi yake hata hivyo ilimfanya pia kulengwa na mashambulio na unyanyasaji, imesema taarifa iliyotolewa na UNESCO  shirika la Umoja wa Mataifa lenye jukumu la kutetea uhuru wa vyombo vya Habari. 

Bi Ressa alichaguliwa kupokea tuzo hiyo ya Uhuru wa wanahabari ya UNESCO / Guillermo Cano kufuatia mapendekezo ya jopo la majaji wa kimataifa la wataalamu wa vyombo vya habari. 

"Mapambano ya Maria Ressa yasiyopingika kwa ajili ya uhuru wa kujieleza ni mfano kwa wanahabari wengine ulimwenguni. Kesi yake ni ishara ya mwenendo wa ulimwengu ambao unawakilisha tishio la kweli kwa uhuru wa vyombo vya habari, na kwa hiyo kwa demokrasia”, amesema Marilu Mastrogiovanni, mwenyekiti wa majaji wa kimataifa wa tuzo hiyo na mwandishi wa habari za uchunguzi kutoka Italia. 

Sherehe ya tuzo hiyo zitafanyika tarehe 2 Mei huko Windhoek, Namibia, wakati wa Mkutano wa kimataifa wa siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani na kuonyeshwa moja kwa moja mtandaoni. 

Kwa mujibu wa UNESCO, Bi Ressa amekamatwa kwa "madai ya uhalifu unaohusiana na kazi yake", na amekuwa chini ya kampeni endelevu ya unyanyasaji wa kijinsia mtandaoni, vitisho na udhalilishaji, ambayo wakati mmoja, ilisababisha yeye kupata wastani wa zaidi ya ujumbe 90 wa chuki kwenye  mtandao wa Facebook. 

Mwanahabari wa zamani wa CNN wa Habari za upelelezi Asia na mkuu wa ABS-CBN News na na Habari za kila siku, Bi Ressa pia alikuwa miongoni mwa kundi la waandishi wa habari aliyetajwa na gazeti la TIME kama “ Mtu mashuhuri wa Mwaka wa Mwaka 2018.” 

Tuzo ya Uhuru wa Vyombo vya Habari ya UNESCO / Guillermo Cano 

Tuzo ya uhuru wa vyombo vya habari ya UNESCO imepewa jina la Guillermo Cano Isaza, mwandishi wa habari wa Colombia ambaye aliuawa mbele ya ofisi za gazeti lake El Espectador huko Bogotá, Colombia, tarehe 17 Desemba 1986. 

Tuzo hiyo ya dola $ 25,000 inatambua mchango bora wa kulinda na kukuza uhuru wa vyombo vya habari, haswa wakati wa hatari. 

Inafadhiliwa na taasisi ya Guillermo Cano Isaza (Colombia), Helsingin Sanomat Foundation (Finland) na Namibia Media Trust. 

Habari kama faida ya umma 

Ukisimamiwa na UNESCO na mwenyeji serikali ya Namibia, Mkutano wa siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani wa 2021 utafanyika kuanzia kesho 29 Aprili hadi 3 Mei chini ya kaulimbiu “Taarifa kama faida ya umma” na pia utazingatia mada nyingine kama uwazi wa majukwaa ya mtandaoni na umuhimu ya kusoma na kuandika habari. 

Mkutano huo pia utashughulikia njia za kukuza na kusaidia vyombo huru vya Habari vinayojitahidi kukabiliana na mgogoro uliozushwa na janga la COVID-19, wakati ambapo vyombo vya habari vya kitaifa na vya mashinani vinakabiliwa na changamoto za kifedha na shinikizo zingine zinazotishia maisha yao na kazi za kazi zao za uandishi. 

TAGS: UNESCO, Siku za UN, Guillermo Cano, Uhuru wa vyombo vya habari