Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Walinda amani wa UN nchini CAR waimarisha ulinzi kufuatia shambulizi la jana Jumatano.

Walinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Afrika ya kati.
UN /MINUSCA
Walinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Afrika ya kati.

Walinda amani wa UN nchini CAR waimarisha ulinzi kufuatia shambulizi la jana Jumatano.

Amani na Usalama

Kufuatia shambulizi la jana asubuhi karibu na Bangui, mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, ambalo lilisababisha mlinda amani mmoja wa Umoja wa Mataifa kutoka Rwanda kupoteza maisha, mpango wa Umoja wa Mataifa wa kuweka utulivu nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, MINUSCA umesema kuwa hali ya jumla inadhibitiwa, ingawa mivutano inaendelea.

Milio ya risasi...walinda amani wa Umoja wa Mataifa wanaonekana wakijibu mashambulizi dhidi ya makundi yenye silaha katika misitu na vilima karibu kabisa na mji mkuu wa Jamhuri ya Afika ya Kati, Bangui.

Walinda amani wa Umoja wa Mataifa wamejiimarisha na kujiweka katika mkao wa utayari katika mji Bangui na katika maeneo yanayozunguka mji huo, kwa kushirikiana na vikosi vya ulinzi na usalama vya Afrika ya Kati, na pia wadau wengine wa usalama. Hii ni kuzuia upenyezaji zaidi wa vikundi vyenye silaha kuelekea mji mkuu, wakilenga kuzorotesha taasisi za kitaifa.  

Usalama wa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa na majengo pia, umeimarishwa. 

Magari ya kijeshi ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa wa MINUSCA yanaonekana kila mahali yakifanya doria katika mitaa ya mji mkuu wa CAR, Bangui. 

Katika upande mwingine ni msafara wa walinda amani wakielekea katika eneo la mstari wa mbele kuimarisha ulinzi katika maeneo yanayotia wasiwasi.  

Wananchi wanaonekana wakiyakimbia makazi yao kwa mamia, wakiwa wamebeba baadhi ya mali zao vichwani, watoto wakitembea wenyewe, na wengine wakibebwa.  

Msafara wa walinda amani umewasili katika eneo la PK12, moja ya vituo vya ghasia ambako mapigano yametokea jana asubuhi.  

Pembezoni mwa barabara anaonekana mmoja wa waasi akiwa amelala chini amezungukwa na askari wa kitaifa na wale wa MINUSCA.  

Luteni Kanali Abdoul Aziz Fall, ni msemaji wa kikosi cha MINUSCA anasema, “hivi sasa hali inasalia kuwa shwari. Mkakati wa vikundi vyenye silaha ambao umejipenyeza Bangui umezuiliwa. Na kwa sasa wanajeshi walioko kwenye eneo, wanadhibiti hali hiyo. " 

Mapema baada ya shambulio la jana, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alirejelea wito wake kwa pande zote kusitisha machafuko na kujihusisha katika majadiliano.