Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

MINUSCA yafadhili ukarabati wa dampo la taka huko Bangui, CAR

Ukarabati wa dampo la taka kwenye mji mkuu wa CAR, Bangui
MINUSCA
Ukarabati wa dampo la taka kwenye mji mkuu wa CAR, Bangui

MINUSCA yafadhili ukarabati wa dampo la taka huko Bangui, CAR

Afya

Nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuweka utulivu MINUSCA umefadhili ukarabati wa dampo la kutupia taka kwenye mji mkuu Bangui kama njia ya kulinda mazingira sambamba na kuboresha maisha ya wakazi wanaozunguka dambo hilo.

Katika kitongoji cha 6 kwenye mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, Bangui [BOONGI] ndiko kunapatikana dampo hilo lenye ukubwa wa hekta 3.7, ambalo ndio eneo kubwa zaidi la kutupa taka jijini humu.
Kazi ya ukarabati wa dampo linaloendeshwa na jiji la Bangui, imeanza mwaka jana wa 2021 kwa lengo la kuhakikisha kuwa linakidhi viwango vya kimataifa, ukarabati ukifadhiliwa na MINUSCA  na kutekelezwa na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya utekelezaji wa miradi, UNOPS. 

Sahon Flan Mkuu wa mazingira MINUSCA anasema “lengo la kwanza ni kuboresha mazingira ya utupaji wa taka ngumu Bangui, kwa sababu ni dampo pekee linalopokea taka za jiji la Bangui na pia MINUSCA. Pili ni kunufaisha wanajamii kwa kuepusha utupaji hovyo wa taka ngumu.”

Mradi huu ulihusisha uhamasishaji wa jamii, ujenzi wa mabwawa ya kuchujia majitaka sambamba, ujenzi wa visima vitatu vya maji na ukarabati wa barabara ya kwenda kwenye dampo.
Narcisse Mbomesse ni msimamizi wa dampo la Kolongo ambaye anasema, « Huwezi kutupa kila taka kwenye dampo kwa sababu hiyo italeta uchafuzi. Sisi tuko hapa kuthibitisha taka zinazoletwa na magari. Kama haziruhusiwi tunalirudisha. Mfano taka za hospitali, za sumu na zile za viwandani, haziruhusiwi. »

Mradi huu uliogharimu dola zaidi ya milioni 2.8 za kimarekani umewezesha pia watendaji kupata mafunzo ya usimamizi wa taka, vifaa vya kujikinga wakati wa kushughulikia taka, huku wakusanya taka nao katika jamii wakijipatia kipato kwa kusomba taka na kupeleka kwenye dampo.
MINUSCA inasema pamoja na kupatia jamii eneo la kutupia taka pia utaepusha jamii na magonjwa kama vile Malaria na kuhara.