Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwandishi wa habari anapouawa, jamii ndiyo inayodhurika- Guterres

Siku ya kimataifa ya kutokomeza ukwepaji sheria wa uhalifu dhidi ya waandishi wa habari
UNESCO
Siku ya kimataifa ya kutokomeza ukwepaji sheria wa uhalifu dhidi ya waandishi wa habari

Mwandishi wa habari anapouawa, jamii ndiyo inayodhurika- Guterres

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Kuelekea siku ya kimataifa ya kutokomeza ukwepaji sheria wa vitendo vya uhalifu dhidi ya waandishi wa habari, kesho tarehe pili mwezi Novemba, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema, uhuru wa kujieleza na vyombo huru vya habari ni muhimu katika kusongesha na kujenga demokrasia sambamba na kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.

Katika ujumbe wake Bwana Guterres amesema licha ya umuhimu huo, “katika miaka ya karibuni kumekuwepo na ongezeko la mashambulizi dhidi ya wanahabari na wafanyakazi wa vyombo vya habari, mashambulizi ambayo yanakwamisha uwezo wao wa kufanya kazi hiyo adhimu, huku wengine wakitishiwa kushtakiwa, kukamatwa, kufungwa jela na kunyimwa uhuru wa kufanya kazi yao na hata uchunguzi wa kufungulia mashtaka wanaotenda uhalifu huo.”

Katibu Mkuu amesema hata matukio ya uhalifu dhidi ya wanahabari wanawake nayo yanaongezeka wakikabilwa na ukatili wa kingono na hata vitisho.

“Waandishi wa habari wanapolengwa, jamii  ndiyo inayolipa gharama. Bila kulinda waandishi wa habari, uwezo wa kuendelea kuhabarishwa na kuchangia katika maamuzi unakwamishwa kwa kiasi kikubwa. Tusipokuwa na waandishi wa habari wenye uwezo wa kufanya kazi zao kwa usalama, tunakabiliwa na dunia iliyokanganyika na yenye habari zisizo za kweli,” amesema Bwana Guterres.

Ni kwa mantiki hiyo amesema katika maadhimisho haya, “hebu na tusimame pamoja kwa ajili ya waandishi wa habari, kwa ajili ya ukweli na kwa ajili ya haki.”

UNESCO na takwimu za mauaji ya waandishi wa habari 2006-2018 

Katika kuadhimisha siku hii, shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni, UNESCO limeangazia zaidi mauaji ya waandishi wa habari duniani kote kuanzia mwaka 2006 hadi 2018.

Ripoti ya UNESCO inasema kuwa takribani asilimia 90 ya wahusika wa mauaji ya waandishi wa habari 1,109 katika kipindi hicho hawajashtakiwa.

Halikadhalika inabainisha ongezeko kwa asilimia 18 la mauaji ya waandishi wa habari katika kipindi cha miaka mitano kuanzia 2014-2018 ikilinganishwa na miaka mitano iliyotangulia.

Eneo hatari zaidi kwa waandishi wa habari ni mataifa ya kiarabu ikiwa na asilimia 30 ya mauaji yote ya wanahabari duniani, ikifuatiwa na Amerika ya Kusini na Karibea asilimia 26 huku eneo la Asia na Pasifiki likiwa la tatu kwa asilimia 24.

Waandishi wa habari wakifuatilia mjadala mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa
UN Photo/Laura Jarriel
Waandishi wa habari wakifuatilia mjadala mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa

Ripoti hiyo inaonesha kuwa katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, 2017-2018, asilimia 55 ya mauaji ya wanahabari yalifanyika kwenye maeneo yasiyo ya mizozo.

“Mwelekeo huu unaonesha kubadilika kwa mwenendo wa mauaji ya waandishi wa habari ambao mara nyingi hulengwa kwa sababu ya kuripoti masuala ya siasa, uhalifu na ufisadi,” imesema ripoti hiyo.

UNESCO imesema mwaka huu hata hivyo imerekodi visa vichache vya mauaji ya waandishi wa habari ikilingainshwa na mwaka jana, ambapo mwaka huu pekee kuna visa 43 ikilinganishwa na 90 katika kipindi kama hicho mwaka jana.

Akizungumzia siku hii, Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO Audrey Azoulay amesema,  UNESCO inalaumu wale wote ambao wanaweka hatarini Maisha ya waandishi wa  habari, wale wote wanaoua waandishi wa habari na wale wote ambao hawafanyi chochote kuzuia ghasia hii. Mwandishi anapouawa isiwe ndio mwisho wa kusaka ukweli.”

Katika kuadhimisha siku hii UNESCO inazindua kampeni kupitia mitandao ya kijamii, #KeepTruthAlive au ukweli usalie hai, ikilenga kuonyesha hatari wanazokumbana nazo waandishi wa habari.

UNESCO inasema asilimia 93 ya waandishi wa habari wanaouwa ni wale wa nyumbani na kuna ramani iliyoandaliwa kuonyesha mauaji ya wanahabari tangu mwaka 1993 ambayo UNESCO ilitoa taarifa kulaani.