Skip to main content

Ulinzi kwa waandishi wa habari unahitaji utashi wa kisiasa: UN

Mwandishi wa habari akichukua tukio kwa video
Unsplash/Jovaughn Stephens
Mwandishi wa habari akichukua tukio kwa video

Ulinzi kwa waandishi wa habari unahitaji utashi wa kisiasa: UN

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Pamoja na kufanya kazi kubwa ya kuhabarisha umma, waandishi wa habari ulimwenguni kote wanakabiliwa na mashambulio yanayohatarisha usalama wao ambapo mashambulio hayo ni pamoja na kauli za chuki, udhalilishaji kwenye mitandao ya kijamii, vurugu, ubakaji na hata mauaji.Ikiwa leo ni siku ya kimataifa ya kukomesha uhalifu dhidi ya waandishi wa habari Umoja wa Mataifa unasema muarobaini wa yote hayo ni utashi wa kisiasa.

Tafiti zilizofanywa na shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu Sayansi na Utamaduni,  UNESCO zimebaini kuwa kati ya mwaka 2006 na 2020, zaidi ya waandishi wa habari 1,200 wameuawa kwa kuripoti habari kwa umma. Utafiti huo umeonesha kuwa kati ya vifo 10 ni kisa kimoja tu ndio muhusika au wahusika wanaadhibiwa.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres anasema dunia lazima ikomeshe uhalifu huu dhidi ya waandshi wa habari ili kuhakikisha uhuru wa kujieleza na upatikanaji wa habari kwa wananchi wote unakuwepo.

“Mwaka jana, kulingana na UNESCO, waandishi wa habari 62 waliuawa kwa kufanya kazi zao tu. Leo tunaadhimisha urithi na mafanikio ya wanahabari waliouawa wakiwa kazini, na tunataka haki itendeke kwa uhalifu unaofanywa dhidi yao. Ninatoa wito kwa Wanachama na jumuiya ya kimataifa kusimama katika mshikamano na waandishi wa habari duniani kote leo na kila siku, na kuonyesha nia ya kisiasa inayohitajika kuchunguza na kushtaki uhalifu dhidi ya waandishi wa habari na wafanyakazi wa vyombo vya habari kwa nguvu zote za sheria. “

Ingawa kwa miaka 5 iliyopita mauaji ya waandishi wa habari yalipungua kwa asilimia 20 lakini takwimu zilizokusanywa mwaka huu wa 2021 zinaonesha uhalifu kwa wanahabari umeongezeka kwa asilimia 87 ikilinganishwa na miaka iliyopita.

Wengi wameuawa katika nchi zao. Kati ya waandishi wa habari 400 waliouawa kutoka 2016 hadi 2020, ni waandishi wa habari 22 pekee sawa na asilimia 6 ndio waliuawa nje ya nchi zao.

Siku hii kwa mwaka huu inaadhimishwa kwa kufanya mjadala wa ngazi za juu kwa mtindo wa mseto wengine watakuwa mkumbini na wengine mtandaoni kwa pamoja wakiangazia jukumu muhimu la huduma za uendeshaji wa mashtaka katika kuchunguza na kushtaki sio tu mauaji, lakini pia vitisho vya unyanyasaji dhidi ya waandishi wa habari.

UNESCO inahusika na masuala ya waandishi wa habari ikiwemo kutoa mafunzo, kufanya tafiti ambazo zinasaidia kutengeneza sera za kuwawezesha waandishi wa habari kuwa wafanisi zaidi na pia kugundua changamoto wanazokabiliana nazo na kuzitafutia ufumbuzi.