Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vyombo huru vya habari ni nguzo ya udumishaji wa demokrasia:UN

Waandishi wa habari wakiwa kazini mjini Kyiv Ukraine
Unsplash/Kate Bezzubets
Waandishi wa habari wakiwa kazini mjini Kyiv Ukraine

Vyombo huru vya habari ni nguzo ya udumishaji wa demokrasia:UN

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Ikiwa leo ni siku ya kimataifa ya kukomesha ukwepaji sheria kwa uhalifu dhidi ya waandishi wa habari Umoja wa Mataifa umesema vyombo huru vya habari ni chachu muhimu ya kuhakikisha utekelezaji wa demokrasia , kufichua mbaya , kukabili dunia hii yenye changamoto na kusongesha ajenda ya maendeleo endelevu SDG’s.

Kupitia ujumbe wake wa siku hii Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema licha ya umuhimu na mchango wao “Bado waandishi wa habari zaidi ya 70 wameuawa mwaka huu sababu ya kutimiza wajibu wao katika jamii. Na uhalifu huu kwa kiasi kikubwa haujapatiwa suluhu , wakati huohuo waandishi wengi wa habari wanashikiliwa vizuizini , vitisho vya kuwafunga vinaendelea, ukatili dhidi yao unaendelea na idadi ya wanaouawa inaongezeka.”

Katibu Mkuu amesisitiza kwamba “Ongezeko la habari potofu, uonevu mtandaoni na matamshi ya chuki, hasa dhidi ya waandishi wa habari wanawake, vinachangia kuwakandamiza wafanyakazi wa vyombo vya habari kote duniani kote.”

Kwa mantiki hiyo ametoa raia kwamba “Tunapoadhimisha miaka 10 tangu kuanzishwa kwa siku hii, natoa wito kwa serikali na jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua zinazofaa kuwalinda wanahabari wetu. Lazima tukomeshe utamaduni wa kawaida wa kutokujali na kuwawezesha waandishi wa habari kufanya kazi yao ambayo ni muhimu.”

Mwandishi mkongwe wa Palestina Shireen Abu Akleh aliyeripoti kwa zaidi ya robo karne ukaliaji wa Isreal huko Palestina
Al Jazeera
Mwandishi mkongwe wa Palestina Shireen Abu Akleh aliyeripoti kwa zaidi ya robo karne ukaliaji wa Isreal huko Palestina

Ukwepaji sheria kwa mauaji ya wanahabri ni asilimia 86

Nalo shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni UNESCO takwimu zake mpya zilizotolewa leo zinaonyesha kwamba duniani kote ukwepaji sheria kwa uhalifu wa mauaji dhidi ya waandishi wa habari uko katika kiwango cha juu sana cha asilimia 86.

Hivyo UNESCO “Inarejea wito wake wa kuchukuliwa kwa hatua zote muhimu na za lazima ili kuhakikisha kwamba uhalifu dhidi ya wanahabari unachunguzwa kwa kina na wahusika wanabinika na kuwajibishwa kisheria.”

Kwa mujibu wa ripoti hiyo mpya ya UNESCO “Kuhusu usalama wa wanahabari na hatari za ukwepaji sheria kwa mwaka 2020-2021” iliyochapishwa leo , takwimu zake zinaonyesha kwamba kiwango cha ukwepaji sheria kimepungua kwa asilimia 9% pekee katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.

UNESCO imekaribisha hatua hizo lakini imeonya kwamba punguzo hilo halitoshi kuweza kufanikisha kukomesha wimbi la machafuko dhidi ya wana habari.

Ripoti hiyo pia inaonyesha kwamba hakuna mahala salama kwa waandishi wa habati.Imeendelea kubainisha kuwa mwaka 2020-2021 miongoni mwa waandishi wa habari 117 waliouawa kwa sababu ya kazi yao , 91 kati yao au asilimia 78% wakiuaw wakiwa nje ya saa za kazi kwa mfano nyumbani, kwenye magari yao au mtaani lakini sio katika kazi maalum.

Pia UNESCO imesema wengi waloiuawa mbele ya wana familia wao wakiwemo watoto wao.