Venezuela barazani, wajumbe wavutana iwapo ni tishio kwa usalama duniani au la!
Vuta nikuvute kuhusu hali inayoendelea nchini Venezuela kwa sasa, imedhihirika leo kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo lilikutana kwenye kikao cha dharura kujadili kinachoendelea wakati huu ambapo kuna mvutano kati ya Rais Nicolas Maduros wa nchi hiyo na Juan Guido rais wa Bunge ambaye amejitangaza rais wa muda wa Venezuela.
Rais Maduros ambaye aliapishwa tarehe 10 mwezi huu wa Januari kuafuatia uchaguzi uliofanyika nchini humo mwezi Mei mwaka jana anaungwa mkono na baadhi ya nchi ikiwemo Urusi ilhali Marekani na mataifa mengine wanamuunga mkono Bwana Guido wakimtaka aitishe uchaguzi mpya.
Mvutano huo umesababisha maandamano nchini Venezuela ambapo akihutubia wajumbe wa Baraza hilo, Mkuu wa Idara ya Siasa kwenye Umoja wa Mataifa Rosemary DiCarlo amesema “hali ya Venezuela inatia wasiwasi mkubwa. Janga hili lililodumu kwa muda mrefu limekuwa na madhara kwa wananchi, kuna mvutano mkubwa kisiasa na kuna hofu kubwa juu ya ongezeko la mahitaji ya kibinamu.”
Amesema janga la Venezuela limeathiri takribani raia milioni 30 ambapo hawana mishahara, kuna uhaba wa chakula, dawa, huduma afya na elimu zimezorota na uzalishaji wa mafuta umeporomoka kwa takribani mapipa laki 5 kwa siku kutoka mwaka 2017 hadi mwaka 2018.
Bi. DiCarlo amesema harakati za kuwezesha mazungumzo kati ya Rais Maduros na upinzani bado hazijazaa matunda “na ghasia zinazondelea zimesababisha vifo vya watu wapatao 20, na wengine wengi wamejeruhiwa.”
Amesema kuna dira tofauti kuhusu mustakabali wa Venezuela hata hivyo, “sote lazima tuongozwe na kile kitakacholeta ustawi kwa wananchi wa Venezuela, na tushirikiane tukidhi mahitaji yao. Tufanye kila tuwezalo kuzuia hali kuwa mbaya zaidi. Lazima tushirikiane tulete suluhu ya kisiasa ambayo itawezesha wananchi kufurahia amani, ustawi na haki za binadamu.”
WAJUMBE WAVUTANA NI WANAOMUUNGA MADUROS NA WALE WA GUIDO
Marekani kwa upande wake iliwakilishwa na Waziri wake wa Mambo ya Nje, Mike Pompeo ambaye kwa kuzingatia kuwa tayari serikali yake inamuunga mkono Bwana Guido, amekebehi nchi zinazomuunga mkono Rais Maduros akisema zinafanya hivyo ili ziweze kukusanya mabilioni ya dola kutokana na vitegauchumi vyao vya hovyo nchini humo.
“Leo natoa wito kwa wajumbe wa Baraza la Usalama waunge mkono mpito wa kidemokrasia na dhima ya Guido katika mchakato huo,” amehitimisha Bwana Pompeo.
Mwakilishi wa kudumu wa Urusi kwenye Umoja wa Mataifa Vasily Nebenzi amesema wao kwa kuiunga mkono Venezuela na Rais Maduros, “kwanza kabisa tunaonyesha kupinga ukiukwaji mkubwa wa maadili ya sheria za kimataifa, hususan, vifungu vya katiba ya Umoja wa Mataifa, ambayo kwa dhahiri inapinga uingiliaji wa masuala ya ndani ya taifa huru.”
Mjumbe mwingine aliyezungumza ni Afrika Kusini ambayo Mwakilishi wake wa kudumu kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Jerry Matthews Matjila, amesema serikali yao haioni kama kinachoendelea Venezuela ni tisho la amani na usalama duniani akisema Rais Cyril Ramaphosa tayari alishampongeza Rais Maduros kwa kuchaguliwa kwake kuongoza nchi yake.
“Kinachoendelea Venezuela ni masuala ya ndani ya nchi na Baraza la Usalama halina mamlaka ya kuingilia mambo hayo na kwa kuzingatia uchaguzi ulifanyika kwa usimamizi wa tume inayotambulika,” amesema Balozi Matijla.
VENEZUELA YAWEKA BAYANA MSIMAMO WAKE
Fursa ikawadia kwa Venezuela kuwasilisha hotuba yake ambapo Waziri wake wa Mambo ya Nje Jorge Arreaza, alipinga katakata hoja zinazotolewa kuhusu ukosefu wa uhuru na demokrasia kwenye nchi yake. Amelaumu Marekani akisema inataka kujenga ukuta mpakani na Mexico na kujenga ukuta wa kiitikadi na kimsingi wanarejesha vita baridi.
Akizungumza huku anaonyesha katiba ya Umoja wa Mataifa, Waziri Arreaza amesema, “kwa jina la Rais Nicolas Maduro, kwa jina la Jamhuri ya Venezuela, kwa jina la wananchi wa Venezuela, na kwa mamlaka ya wengi Venezuela, taasisi na jamii, napenda kusisitiza kuwa Venezula, kama ilivyotajwa kwenye katiba hii, ni huru, na itasalia huru na hakuna mamlaka yoyote bila kujali ukubwa wake inaweza kuamuru mwelekeo au mustakabali wa nchi yetu.”
MUUNGANO WA ULAYA NAO WAKANA KUTAMBUA UCHAGUZI WA MEI 2019
Punde baada ya kikao hicho, Sir Alan Duncan wa Uingereza akizungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya Muungano wa Ulaya, EU, amesema hawatambui uchaguzi uliofanyika mwezi Mei mwaka jana nchini Venezuela ambapo Rais Maduros alichaguliwa kwa asilimia 68 kuongoza nchi yake kipindi cha pili cha miaka 6. Amesema uchaguzi huo haukuwa huru na wa haki.
Badala yake amesema wanaunga mkono Bunge la Venezuela "ambacho ndio chombo cha kidemokrasia na kisheria. Tunaamni kuwa suluhu ya amani na jumuishi ndio muarobaini wa mkwamo wa sasa na zahma ya kijamii ambayo imesababisha. EU inataka kuitishwa mara moja kwa uchaguzi huru kwa mujibu wa viwango vya kimataifa vya demokrasia na katiba ya Venezuela. Bila kufanya hivyo, EU itachukua hatua zaidi ikiwemo kutambua uongozi wa nchi kwa mujibu wa kifungu namba 233 cha Katiba ya Venezuela."
Kipengele hicho ni kile kinachompatia madaraka ya kuongoza nchi Rais wa Bunge la nchi hiyo.
Hii ni mara ya kwanza kabisa kwa Baraza la Usalama kuwa na kikao mahsusi kuhusu Venezuela. Nyakati nyingine Venezuela ilijadiliwa kama ajenda lakini si kama sababu mahsusi ya kikao kama leo.