Kuvuka baharí ya mediterania imekuwa kama tiketi ya kifo:UNHCR
Ikiwa ni miaka mitatu tangu picha za kutisha za mwili wa mtoto mdogo, Alan Kurdi, akiwa katika ufukwe wa bahari nchini Uturuki zisambae, ripoti mpya ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi, UNHCR inaonyesha kuwa wakati huu kuvuka baharí ya Mediterania imekua hatari zaidi inayosababisha vifo kuliko wakati mwingine wowote.
Ripoti mpya ya UNHCR, iliyopewa jina “safariza kukatisha tamaa” inaonyesha kuwa watu zaidi ya 1,600 wamefariki dunia au kutoweka wakijaribu kwenda Ulaya mwaka huu kupitia baharí hiyo. Ikiongeza kuwa ingawa idadi ya watu wanaosafiri kuingia Ulaya imepungua lakini idadi ya vifo imepanda sana.
Mediterania ya kati, ripoti inaonyesha mtu mmoja kati ya 18 alifariki dunia au kupotea kwa waliofanikiwa kufika Ulaya kati ya miezi ya Januari na Julai 2018, ikilinganishwa na kifo cha mtu mmoja kwa kila watu 42 waliovuka kipindi cha mwaka wa 2017.
Mkurugenzi wa Ofisi ya UNHCR tawi la Ulaya, Pascale Moreau, amesema kuwa , ripoti hii kwa mara nyingine inadhihirisha kuwa Mediterania ni moja wa vivuko hatari zaidi duniani.Ameongeza kuwa kutokana na idadi ya wanaowasili kuingia Ulaya kupungua, hii sio tena mtihani wa endapo Ulaya itaweza kumudu idadi ya wahamiaji bali ni endapo Ulaya ina utu wa kuokoa maisha.
Miezi michache iliyopita , UNHCR pamoja na shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji IOM,wametoa wito wa kuwepo kwa mtazamo wa kikanda wa uokozi na kuwapeleka ufukweni watu ambao wako katika shida kwenye baharí ya Mediterania.
Pia UNHCR imeliomba bara Ulaya kuimarisha mpango wa njia salama na fursa kwa wakimbizi na waomba hifadhi , kuondoa vikwazo dhidi ya watu hao kuunganishwa tena na familia zao na pia kusaidia kupatikana kwa njia mbadala ya ile hatarishi.