Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yasikitishwa na vifo vya wakimbizi na wahamiaji bahari ya mediteranea

Wasaka hifadhi wakiokolewa na meli ya ubelgiji katika bahari ya mediteranea
Frontex/Francesco Malavolta
Wasaka hifadhi wakiokolewa na meli ya ubelgiji katika bahari ya mediteranea

UNHCR yasikitishwa na vifo vya wakimbizi na wahamiaji bahari ya mediteranea

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, limeelezea kusikitishwa na ripoti za vifo vya  watu takriban 170 ambao wamefariki dunia au hawajulikani waliko kufuatia  ajali za meli mbili tofauti katika bahari ya mediteranea.

UNHCR kupitia taarifa iliyochapishwa kwenye wavuti wake, imesema watu takriban 53 wamefariki dunia katika bahari ya  Alborán, magharibi mwa  Mediteranea, kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa mashirikia yasiyo ya kiserikali, NGOs. 

Kwa mujibu wa taarifa, mmoja wa manusura aliokolewa na boti ya wavuvi baada ya kukaa baharini kwa zaidi ya saa 24 na anapata matibabu nchini Morocco. Timu za uokozi kutoka Morocco na Hispania zimekuwa zikisaka boti hiyo lakini bado haijapatikana.
 
Askari wa majini kutoka Italia wameripoti kuwa kuna boti nyingine imepata ajali Mediteranea kati ambapo kulipatikana manusura watatu ambao wamepelekwa kupata matibabu Lampedusa, ambapo wameripoti kuwa kuna watu 117 ambao huenda wamefariki dunia au hawajulikani waliko tangu walipo ng’oa nanga kutoka Libya
UNHCR haijaweza kuthibitisha idadi kamili ya vifo kufuatia ajali za meli hizo mbili.

Waokoaji wa kikosi cha wanamaji cha Italia wakiokoa wahamiaji kwenye bahari ya Mediteranea
Italian Coastguard/Massimo Sestini
Waokoaji wa kikosi cha wanamaji cha Italia wakiokoa wahamiaji kwenye bahari ya Mediteranea

Kamishna mkuu wa UNHCR, Filippo Grandi, amesema, “hatuwezi kuendelea kufumba macho wakati watu wengi wanafariki dunia mlangoni mwa Ulaya, kila hatua inapaswa kuchukuliwa ili kuokoa maisha ya watu wanaovuka kupitia bahari".

Mwaka 2018 watu 2,262 walipoteza maisha wakijaribu kufika Ulaya kupitia bahari ya Mediterranea.
UNHCR  ina wasiswasi kuwa hatua za mataifa zinazuia NGOs kutoshiriki operesheni za kuokoa watu na hivyo kutaka vikwazo viondolewe.
 
Wakati huo huo UNHCR imesema hatua zaidi zinahitajika kuzuia wakimbizi na wahamiaji kuchukua safari hatarishi na kwamba njia salama na zinazozingatia sheria zinapaswa kuwepo kufika Ulaya kwa wale wanaokimbia vita na mateso ili kuepukana na vishawishi kutoka kwa wasafirishaji haramu.