Nchi za Ulaya unganeni kuwasaidia wanaopatwa na masaibu katika baharí ya Mediterania.

22 Januari 2019

Mashirika ya Umoja wa Mataifa ikiwemo lile la kuhudumia wakimbizi UNHCR na lile linaloshughulikia wahamiaji IOM hii leo mjini Geneva Uswisi wametoa wito kwa nchi za Ulaya kuungana katika kushughulikia masaibu yanayowakumba watu wanaojaribu kuvuka baharí ya mediterania ili kutafuta hifadhi katika nchi nyingine duniani hususani za bara Ulaya.

Wito huo umetolewa wakati huu amapo kuna ongezeko la matukio ya kuokolewa na kuzama kwa wahamiaji  katika bahari ya Mediterania katika siku za karibuni ambayo ni ushahidi kuwa nchi za bara Ulaya zinatakiwa kuchukua hatua za haraka kusaidia. Mathalani mwishoni mwa wiki iliyopita, takribani watu 170 walisadikiwa kuzama katika matukio tofautitofauti katika fukwe za Libya na Morocco.

Katika tukio moja ijumaa iliyopita, zaidi ya watu 100 wanaaminika wamepoteza maisha katika maji ya Libya ambako ulinzi wa fukwe umesitishwa kutokana na uhaba wa mafuta.

Msemaji wa IOM Joel Millman anaeleza, “watu watatu waliokolewa na helikopita ya jeshi la anga la Italia maili 50 kutoka ufukwe wa Libya na kuwaleta Lampedusa Italia. Wafanyakazi wa IOM walizungumza na manusura ambao walisema boti ilikuwa imebeba watu 120. Kwa kuzingatia ushuhuda huo, IOM inakadiria kuwa wati 117 wamepotea na labda wamezama bahatrini kabla ya huduma ya uokozi kuwafikia. Kwa mujibu wa manusura, wanawake 10 mmoja akiwa mjamzito pamoja na Watoto wawili walikuwa kwenye boti hiyo”

Katika taarifa mwendelezo wa ufuatiliaji, IOM inaripoti kuwa wahamiaji 150 wamerejeshwa Libya na kuwekwa kizuizini baada ya kuokolewa na meli ya mizigo.

UNHCR imethibitisha kuwa wahamiaji na wakimbizi wanaoshikiliwa nchini Libya wameathirika katika vituo rasmi na visivyo rasmi wanamohifadhiwa, wengi wakiwa na njaa kali.

Shirika hilo la kuhudumia wakimbizi limesisitiza kuwa Libya haina bandari salama za kuwahifadhi wanaokolewa na hapo likatoa wito wa kuungana kwa nchi na serikali za Ulaya kuwasaidia watu wanaohama.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud