Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nchi za kiarabu anzisheni mifumo jumuishi ili kupata maendeleo- IMF

Jiji la Beirut, Lebanon
World Bank/Dominic Chavez
Jiji la Beirut, Lebanon

Nchi za kiarabu anzisheni mifumo jumuishi ili kupata maendeleo- IMF

Ukuaji wa Kiuchumi

Mataifa ya kiarabu yamehimizwa kubuni mifumo jumuishi kwa ajili ya maendeleo.

Wito huo umetolewa leo mjini Beirut Lebanon na  Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya kati na Asia ya kati katika shirika  la fedha duniani -IMF Jihad Azour kwenye mkutano wa kiuchumi wa mataifa ya kiarabu.

Amesema hatua hiyo ni muhimu kwa kuwa eneo la uarabuni ndilo lenye idadi kubwa ya vijana wasio na ajira duniani akisema kuwa vijana zaidi ya milioni 27 watakuwa wakitafuta kazi  katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Amewaambia wajumbe wa mkutano huo kuwa, mabadiliko katika mifumo inayosaidia ukuaji jumuishi yanaweza kusaidia  kuleta mafanikio makubwa.

 

Mji wa Doha,Qatar
Milton Grant
Mji wa Doha,Qatar

 

Bwana Azour ametaja mabadiliko hayo kuwa ni pamoja na kusaidia makundi yaliyotengwa au yaliyo pembezoni ili yaweze kuwa sehemu ya uchumi. Kwa mantiki hiyo amesema sera ni lazima ziridhiwe ili kujumuisha vijana, wanawake na wakazi wa vijijini kwenye nguvu kazi ya taifa kwa kuwaandaa kwa kazi zinazofaa.

“Ujumuishi wa kifedha ikiwemo matumizi ya teknolojia katika sekta ya fedha ni mbinu muhimu ya kuwezesha raia kwa kuwa takribani asilimia 70 ya wakazi wa ukanda huo wa mashariki ya kati na Asia ya Kati hawana akaunti za benki,” amesema Bwana Azour.

Hatua nyingine kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo wa IMF ni kutunga sera za fedha zinazowekeza katika rasilimali watu na miundombinu.

Amesema hatua hiyo inawezekana iwapo sera hizo za fedha zitabuniwa upya ili kuhakikishe makusanyo yote ya fedha za umma yanatumika kuboresha miundombinu ya kijamii ikiwemo elimu, afya, huduma za pensheni na barabara.

 

Jiji la Cairo Misri
Dominic Chavez/World Bank
Jiji la Cairo Misri

 

Amewasifu vijana wa eneo hilo akisema  wana vipaji na iwapo watapewa wanafasi watadhihirisha umuhimu wa kukuza uchumi jumuishi kwa mafanikio ya muda mrefu ya kanda hiyo.

Bwana Azour, amesema kuwa IMF inaamini kuwa jamii huimarika  ikiwa kila mmoja wake atapata nafasi na ndio maana ni muhimu kwa nchi za kanda ya kiarabu kuwekeza katika  vijana  wenye vipaji na kutumia vema nafasi za mawasiliano kuwasiliana na maeneo mengine ya dunia.