Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Othman ateuliwa tena kuongoza uchunguzi wa kifo cha Hammarskjöld

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Dag Hammarskjöld akihutubia mkutano wa waandishi wa habari katika Makao makuu ya Umoja wa Mataifa tarehe 24 Machi 1960. Picha: UM

Othman ateuliwa tena kuongoza uchunguzi wa kifo cha Hammarskjöld

Amani na Usalama

Mohammed Othman Chande wa Tanzania ateuliwa tena kuendelea kuongoza uchunguzi wa kifo cha  Dag Hammarskjöld

Kwa mara nyingine tena Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amemteua Jaji Mkuu mstaafu wa Tanzania Mohammed Chande Othman kuongoza jopo la uchunguzi wa kifo cha Dag Hammarskjöld.

Hammarskjöld ambaye alikuwa Katibu Mkuu wa pili wa Umoja wa Mataifa alifariki dunia tarehe 18 Septemba mwaka 1961 kwenye ajali ya ndege huko Ndola, Zambia wakati akiwa safarini kusaka amani kwenye iliyokuwa Zaire sasa ikitambuliwa kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

Uteuzi wa Othman huo ni kwa mujibu wa azimio namba 72/252, la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ambapo uteuzi wa Bwana Othman unajumuisha pia jopo la wajumbe aliokuwa nao awali.

Image
Marehemu aliyewahi kuwa Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Dag Hammarskjöld.(Picha:UM/AF/NICA ID:60990)

Ikumbukwe kuwa Katibu Mkuu awali alimteua Bwana Othman kuwa mjumbe wa jopo la watu mashuhuri kwa jukumu hilo la uchunguzi ambapo ripoti iliwasilishwa mbele ya Baraza Kuu mwezi Septemba mwaka jana.

Ripoti ilihitimisha kuwa bado kuna masuala yaliyosalia kuhusu uwezekano kuwa pengine shambulio kutoka nje ya ndege hiyo linaweza kuwa sababu ya ndege yao kuanguka.

Katibu Mkuu amesihi nchi wanachama kutoa ushirikiano kwa Othman na jopo lake ili waweze kutekelekeza jukumu lao la uchunguzi zaidi hivyo mwenye taarifa zaidi awapatie.