Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi wanaofika mpakani mwa Sudan na Sudan Kusini wanasaidiwa na IOM kusafiri

Wakimbizi wanaofika mpakani mwa Sudan na Sudan Kusini wanasaidiwa na IOM kusafiri

Pakua

Wananchi waliokimbia makazi yao kutokana na vita inayoendelea nchini Sudan wanasaidiwa nchini Sudan Kusini na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji IOM ambalo limeeleza zaidi ya watu nusu milioni wamevuka mpaka na kuingia eneo la Renk na sasa wanawapatia usaidizi wa usafiri ili kufika kwenye maeneo watakayopata usaidizi. 

Maelfu ya watu wanavuka mpaka katika eneo la Renk nchini Sudan Kusini ambako IOM imesema lina hali ngumu kwani hakuna maji, chakula, usafiri wala usalama wa aina yeyote na ni eneo lililo mbali. Maelfu ya watu wameovuka mpaka wanaonekana kuwa ni dhaifu. Wengi wao wana kiwewe. 

Msemaji wa IOM Afrika Mashariki Yvonne Ndege anasema wamezungumza na wanawake, watoto na wazee ambao wamekimbia ghasia na wametumia wiki na miezi, kujaribu kufikia mpaka huo.

“Hali waliyoielezea, waliyo yashuhudia ni ya kutisha kabisa. Wengine wanasema walikimbia vurugu. Wengine wanasema walikimbia risasi. Wengine wanasema walifanyiwa ukatili wa kijinsia wakiwa safarini. Wengine wanasema walitumia siku nyingi sana msituni wakijaribu kufikia mpaka huu. Tulizungumza na familia moja, mama akiwa na binti zake wawili na mama yake mwenyewe, ambaye alisafiri kutoka mji mkuu wa Sudan, Khartoum, mpaka kufika mpaka huu na kuvuka salama. Aliumia sana, alifadhaika sana. Lakini anamshukuru Mungu kwamba alikuwa ametoroka na uhai wake.”

Msemaji huyo wa IOM imeeleza wameandaa zaidi ya safari za ndege 1,200 vile vile kuna usafiri wa maji ambapo wakimbizi wengine watasafirishwa kwa siku tatu kutoka Renk kupitia mto Nile mpaka kufika Malakal mji mkuu wa jimbo la Upper Nile. 

“Usaidizi huu ni muhimu kabisa kwa sababu kile IOM na mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa hawataki, ni kambi za wakimbizi kuibuka katika eneo hili kwa sababu liko mbali sana. Hakuna miundombinu. Hakuna hospitali, hakuna vifaa vya matibabu. Hakuna rasilimali za aina yoyote kwa watu.”

Pamoja na usaidizi huo unaotolewa na IOM pamoja na mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa bado Kuna wasiwasi mkubwa juu ya hatari ya kuibuka kwa magonjwa, njaa na vurugu zaidi.

IOM imekuwa ikifanya ukaguzi wa kimatibabu na kutoa chanjo kabla ya kuwasafirishwa.

Audio Credit
Evarist Mapesa
Audio Duration
2'41"
Photo Credit
© IOM/Elijah Elaigwu