Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali DRC si hali tena, mashirika ya UN yataka msaada zaidi na ulinzi kwa raia

Hali DRC si hali tena, mashirika ya UN yataka msaada zaidi na ulinzi kwa raia

Pakua

Mashirika ya Umoja wa Mataifa lile la kuhudumia watoto UNICEF na la mpango wa chakula duniani WFP leo yametoa wito wa kuchukuliwa hatua mara moja kuwalinda watoto na familia zao waliojikuta katikati ya machafuko yanayoendelea Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, huku lile la kuhudumia wakimbizi UNHCR likielezea wasiwasi mkubwa kuhusu mustakbali wa zaidi ya raia milioni 7 waliotawanywa na kuomba msaada zaidi kutoka jumuiya ya kimataifa.

Kwamujibu wa WFP na UNICEF idadi kuwa ya watu wakiwemo watoto wamejeruhiwa au kuawa karibu na makazi ya kambi za wakimbizi na yametoa wito kwa pande zote katika mzozo kuwalinda raia na kuruhusu mashirika ya misaada ya kibinadamu  kufanya kazi yao.

Mashirika hayo yamesema mapigano ya sasa yamesababisha janga kubwa la kibinadamu na katika wiki mbili zilizopita yamesogea kilometa 25 mwagharibi mwa mji wa Goma kuelekea Sake ambako watoto na familia zao sasa wamezingirwa na mapigano.

Mwakilishi wa UNICEF nchini DRC Grant Leaity amesema "Watoto nchini DRC wanahitaji amani sasa. Tunatoa wito kwa watoto kulindwa katika vita hivi na kukomesha ukatili huu kupitia juhudi mpya za kutafuta suluhu za kidiplomasia. Tuna wasiwasi mkubwa kuhusu usalama wa watoto na familia zao walio ndani na karibu na kambi za Goma.”

Nalo shirika la UNHCR limesema  mapigano haya yamesababisha msongamano mkubwa wa watu kwenye kambi za wakimbizi ambazo tayari zimejaa pomoni watu waliofurushwa makwao. 

Watu zaidi ya 214,000 wamejiunga na watu wengine 500,000 ambao tayari walikimbia hadi maeneo ya karibu na Goma.

Shirika hilo limesema linatiwa hofu kubwa kwani hadi sasa zaidi ya watu milioni 7 wametawanywa nchini DRC ukijumuisha na wengine nusu milioni ambao ni wakimbizi na wengi wanakabiliwa na changamoto za hali duni ya malazi, huduma mbovu za usafi na fursa finyu za kujipatia kipato.

Ili kushughulikia changamoto hizo na nyingine nyingi za kibinadamu mwaka huu 2024 ombi la dola bilioni 2.6 lilizinduliwa wiki hii kusaidia watu milioni 8.7 wanaohitaji msaada wa kibinadamu DRC.

Lakini jana pia UNHCR na washirika wake walizindua mkakati wa kikanda wa ulinzi na msaada kwa DRC unaohitaji dola milioni 668 kusaidia karibu wakimbizi milioni 1 na jamii zinazowahifadhi hasa nchini Angola, Burundi, Jamhuri ya Congo, Rwanda, Uganda, Tanzania na Zambia.

Audio Credit
Flora Nducha
Sauti
2'31"
Photo Credit
© WFP/Michael Castofas