Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukanda wa Gaza: Uvamizi wa Rafah itakuwa ni janga lisiloelezeka, yaonya UN

Ukanda wa Gaza: Uvamizi wa Rafah itakuwa ni janga lisiloelezeka, yaonya UN

Pakua

Madaktari wa Umoja wa Mataifa leo wamesema wanahofia janga la kibinadamu lisiloelezeka endapo uvamizi kamili wa jeshi la Israeli utatokea Rafah kusini mwa Gaza ambako maelfu ya maelfu ya watu wamekimbilia tangu kuzuka kwa mzozo huu mpya Oktoba 7 mwaka jana. 

Likiunga mkono wasiwasi huo ulioelezwa pia na mratibu Mkuu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja na mkuu wa shirika la kuratibu misaada ya kibinadamu OCHA, Mataifa Martin Griffiths kwamba kushambuliwa kwa Rafah "kunaweza kusababisha mauaji makubwa” Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa Duniani WHO limesema kila liwezekanalo linapaswa kufanyika kuzuia mashambulizi hayo huku pia likikanusha vikali madai ya ushirikiano wa miaka mingi na washirika wasio wa afya ndani au chini ya hospitali za Gaza.

Dkt. Teresa Zakaria Msimamizi wa matukio wa WHO katika eneo linalokaliwa la Palestina amesema, "Hatuwezi kupaza sauti zaidi kukanusha kwamba hakuna ushirikiano kati ya WHO na taasisi nyingine yoyote katika sekta ya afya, washirika wa afya, na katika wizara ya afya ya Gaza ambao tunashirikiana nao," 

Naye Dkt Rik Peeperkorn, Mwakilishi wa WHO katika eneo linalokaliwa la Palestina akizungumza kutoka Gaza amesisitiza kwamba hospitali "hazipaswi kuendeshwa kijeshi na kwamba macho yote sasa yako kwenye uhasama na mashambulizi makubwa yanayohofiwa huko Rafah. Unaona hofu inayowakabili watu. Na watu kila wakati huja na maswali wanauliza tunaweza kufanya nini?"

Maendeleo hayo yanakuja wakati vituo vya hospitali "vimelemewa na kutokuwa na uwezo  na viko ukingoni kusambaratika kabisa",amesema Dkt Peeperkorn huku akibainisha kuwa Wagaza milioni 1.5 sasa wamesongamana kwenye mahema ya muda na makazi ya UNRWA kila kona ya mkoa wa Rafah.

Nao wataalam huru wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa leo wameonya juu ya athari mbaya za mzozo huo Gaza kwa maisha ya waandishi wa habari wakisema, "Tunasikitishwa na idadi kubwa ya waandishi wa habari na wafanyakazi wa vyombo vya habari ambao wameuawa, kushambuliwa, kujeruhiwa na kuzuiliwa katika eneo la Palestina linalokaliwa hasa huko Gaza, katika miezi ya hivi karibuni wakipuuza waziwazi sheria za kimataifa. Tunalaani mauaji, vitisho na mashambulizi yote dhidi ya waandishi wa habari na tunatoa wito kwa pande zote kwenye mzozo kuwalinda." 

Audio Credit
Flora Nducha
Audio Duration
2'35"
Photo Credit
© UNICEF/Eyad El Baba