Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nchini Burundi mbinu ya mashangazi na baba wa shuleni yaepusha watoto na kejeli kutoka kwa wenzao

Nchini Burundi mbinu ya mashangazi na baba wa shuleni yaepusha watoto na kejeli kutoka kwa wenzao

Pakua

Nchini Burundi shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limechukua hatua kuhakikisha watoto wakimbizi wanaorejea nchini humo wanaweza kuendelea na elimu bila uoga na jakamoyo hasa pale wanapokumbana na vizuizi vya tofauti ya lugha waliyotumia ukimbizini na ile inayotumika nyumbani walikorejea. 

Hebu fikiria baada ya machungu ya ukimbizini, unarejea nyumbani nako shuleni unakumbwa na kejeli kisa tu matamshi ya lugha utumiayo ni tofauti na yale ya wenzako darasani. 

Pelouse Nibitanga huyu, ambaye amerejea Burundi kutokea Rwanda ni mwanafunzi wa darasa la saba katika shule ya msingi Kamena iliyoko mkoa wa Kirundo kaskazini mwa Burundi barani Afrika anathibitisha.  

Anasema niliporejea hapa kutangamana hakukuwa rahisi. Kwani wanafunzi wengine walinicheka na kunikejeli kwa matamshi yake ya lugha darasani. Katika mazingira hayo kufaulu ilikuwa ni changamoto. 

Kupitia mradi wa kuweko kwa mashangazi na wababa wa shuleni, wanafunzi kama Pelouse na wale waliokuweko walipatiwa msaada sio tu wa kielimu bali pia kisaikolojia wa kuwawezesha kuishi na kusoma kwa utangamano. Mwalimu Sandrine Kamutako ni miongoni mwa washauri nasaha na mashangazi wa shuleni. 

“Usaidizi wa kisaikolojia na kijamii unaongeza zaidi imani ya mtoto kwa mwalimu na mnasihi wake. Mbinu hii ni nzuri kwani inasaidia wanafunzi kuwa na tabia nzuri. Na pia hujenga kuaminiana kati ya mwalimu na mwanafunzi.” 

Pelouse anathibitisha hilo akisema “shukrani sana kwa ushauri nasaha kwani nilianza kufuatilia masomo vizuri sana na nilimaliza darasa la 6 na sasa nimejiunga na darasa la 7. Sina tena aibu na ninafurahia masomo na wanafunzi wengine. Utangamano wangu unastawi vizuri. Inafurahisha mno.” 

Mafunzo hayo ya kuleta utangamano yamekuwa na manufaa kwa wanafunzi zaidi ya 18, wakiwemo zaidi ya 7,000 waliorejea Burundi kutoka ukimbizini. 

Shule nufaika na mafunzo hayo pia zimenufaika na miradi mingine kama ya ujenzi wa miundombinu ya kuvuna maji ya mvua, madarasa na mafunzo kwa walimu zaidi ya 1,500, UNICEF Burundi ikisema yote yamewezekana kufuatia ufadhili kutoka Muungano wa Ulaya, EU. 

Audio Credit
Assumpta Massoi
Sauti
2'21"
Photo Credit
Photo: OCHA Burundi / Ana Maria Pereira