Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hospitali zazidi kuzidiwa uwezo, wagonjwa sakafuni katika hospitali - Mzozo Gaza

Hospitali zazidi kuzidiwa uwezo, wagonjwa sakafuni katika hospitali - Mzozo Gaza

Pakua

Ikiwa leo ni siku ya 93 tangu mapigano yaanze huko Ukanda wa Gaza kati ya jeshi la Israel na wanamgambo wa kipalestina waliojihami, likiwemo kundi la Hamas, mashirika ya Umoja wa Mataifa ya usaidizi wa kiutu yanazungumzia uwepo wa idadi kubwa ya vifo miongoni mwa wanawake na watoto huku yakisihi timu za madaktari ziruhusiwe kuingia eneo la Gaza ili ziendelee na jukumu la kuokoa maisha.  

Naanzia eneo la kati mwa Gaza ambako huko shirika la Umoja wa Mataifa la Afya, WHO limeonya kuwa madaktari katika hospitali pekee inayotoa huduma kwenye jimbo la Deir al Balah ilibidi jana Jumapili waache kutoa huduma baada ya kupokea amri ya kutakiwa kuondoka eneo hilo kutokana na mashambulizi yanayoendelea kufanywa na jeshi la Israel.  

Na kwenye hospital ya Al-Aqsa ambako timu ya WHO ilipeleka vifaa vya matibabu kusaidia wagonjwa 4,500 wanaohitaji huduma ya kusafisha figo na wengine 500 wanaokabiliwa na kiwewe, idadi ya madaktari waliosalia ni watano pekee.  

Kupitia mtandao wa X, Afisa wa WHO anayehusika na masuala ya dharura ya afya Sean Casey alichapisha video inayoonesha heka heka kwenye hospitali hiyo ya Al- Aqsa, wagonjwa wakiwa wamefurika sakafuni, madaktari wakiwapatia tiba hapo hapo, huku damu imetapakaa, na mamia ya wagonjwa wengine wakifikishwa hapo kwa ajili ya matibabu.  

Dkt, Tedros Ghebreyesus ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa WHO naye kupitia mtandao wa X akasema hospitali ina mahitaij makubwa, kama vile wahudumu wa afya, vitanda lakini wafanyakazi wa Al- Aqsa wanasema jambo muhimu zaidi kwao, wagonjwa na familia ni kulindwa dhidi ya mashambulizi ya makombora na uhasama ukome.  

Huku mashambulizi yakiendelea shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoot, UNICEF linasema magonjwa nayo yanashamiri kwani kila siku kuna wagonjwa wapya 3,200 wa kuhara miongoi mwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano.  

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya dharura, OCHA imenukuu takwimu mpya kutoka Wizara ya Afya ya Gaza zikionesha kuwa kati ya Ijumaa na jana Jumapili wapalestina 225 wameuawa na 300 wamejeruhiwa  huku jeshi la Israel likiripotikuwa tangu lianze operesheni za ardhini, askari wake 174 wameuawa na wengine zaidi ya 1,000 wamejeruhiwa. 

Audio Credit
Assumpta Massoi
Sauti
2'16"
Photo Credit
WHO Video