Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sikuwa nataka kurejea nchini mwangu Sudan Kusini - Mkimbizi kutoka Sudan

Sikuwa nataka kurejea nchini mwangu Sudan Kusini - Mkimbizi kutoka Sudan

Pakua

Wakati maelfu ya wananchi wakikimbia machafuko nchini Sudan mashirika ya Umoja wa Mataifa nayo yana haha huku na kule kuhakikisha wanatoa usaidizi kwa wakimbizi hao. 

Tangu kuibuka kwa mzozo nchini Sudan miezi sita iliyopita, takriban watu milioni 6 wamelazimika kuyakimbia makazi yao wakisaka hifadhi katika nchi jirani zikiwemo Jamhuri ya Afrika ya Kati, Chad, Misri, Ethiopia na Sudan Kusini. 

Kumekuwa na idadi kubwa ya wakimbizi wa Sudan Kusini ambao walikimbilia Sudan lakini sasa wamamua kurejea katika nchi yao. Mmoja ya watu hao ni Umjuma Achol Mtu mwenye umri wa miaka 26, Mwaka 2016 alikimbia ghasia za kikatili katika kijiji chake cha Bentiu, lakini mgofor unaondelea hivi sasa Sudan umemrejesha Sudan Kusini.

“Sikuwa nataka kurejea nyumbani Sudan Kusini kwa sababu ya jinsi tulivyoondoka mwaka 2016. Hali ilikuwa mbaya sana, kumbukumbu bado zinarejea akilini mwangu. Nilikuwa Bentiu vita vilipozuka. Ilitubidi kutembea kilomita 14 kutoka Bentiu hadi Gambella ili kupata usalama. Baadaye tuliishi nchini Sudan.”

Ukosefu wa fedha, ufikiaji duni wa watu, na miundombinu duni vinaleta changamoto kubwa kwa mashirika ya Kimataifa kutoa misaada kwa wakimbizi kama anavyoeleza Jimmy Ogwang, Afisa wa Mashinani wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia wakimbizi UNHCR nchini Sudan Kusini.

“Mvua imeanza kunyesha, sasa tuna changamoto ya barabara hasa kwa wakimbizi, wataathirika kwa sababu kutakuwa hakupitiki maana eneo hili hufurika wakati mvua inanyesha. Kwa hivyo kuna uwezekano mkubwa wa watu kukaa kwa muda mrefu hapa, na watu wakikaa kwa muda mrefu basi kutakuwa na msongamano.” 

Timu za UNHCR, zikiwa pamoja na wadau wengine ziko katika vituo vya kuvuka mpaka nchini Sudan Kusini kufuatilia na kuwasaidia wanaowasili hasa wakimbizi wa Sudan Kusini wanaorejea.

Wameanzisha vituo kwa ajili ya wasafiri ambapo wahamiaji wapya hupewa chakula, maji na malazi katika makazi ya jumuiya huku wakiwatafutia usafiri wa kuelekea maeneo yao ya nyumbani au maeneo mengine wanayopendelea. 

UNHCR pia inasaidia familia kuanzisha mawasiliano na jamaa zao ndani ya Sudan Kusini ili waweze kuunganishwa tena.

Audio Credit
Thelma Mwadzaya
Audio Duration
2'29"
Photo Credit
© WFP/Eulalia Berlanga