Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

26 SEPTEMBA 2023

26 SEPTEMBA 2023

Pakua

Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina ambapo hivi karibuni Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC Félix-Antoine Tshisekedi Tshilombo alihutubia mjadala mkuu wa mkutano wa 78 wa Baraza  Kuu la Umoja wa Mataifa na kutangaza kuwa uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika nchini humo mwishoni mwa mwaka huu, utafanyika kama ilivyopangwa. Alisema tayari Tume Huru ya Uchaguzi nchini DRC, CENI [SENI] imeshachapisha majina ya wagombea na michakato mingine inaendelea. Kufuatia kauli hiyo, mwandishi wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa nchini humo, George Musubao amezungumza na msemaji wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani DRC, MONUSCO ofisi ya Beni-Lubero jimboni Kivu Kaskazini Tobi Okala, kufahamu MONUSCO inafanya nini kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa uhuru na amani. Pia tunakuletea habari kwa ufupi na mashinani, baki nasi!

  1. Hii leo Mjadala Mkuu wa mkutano wa 78 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa umekunja jamvi ambapo viongozi na wawakilishi kutoka nchi 15 wamehutubia wakiwemo kutoka India, Zambia na Morocco. Mjadala huo umefungwa na Rais wa Baraza Kuu Balozi Dennis Francis.
  2. Siku ya Kimataifa ya Kutokomeza Kabisa Silaha za Nyuklia inatukumbusha kwamba wakati ujao wenye amani unategemea kukomeshwa kwa tishio la nyuklia, ndivyo António Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alivyouanza ujumbe wake mahususi kwa ajili ya siku hii inayoadhimishwa kila mwaka tarehe 26 Septemba. Kwa msingi huo Guterres anatoa wito mataifa yenye silaha za nyuklia yaongoze kwa kutimiza wajibu wao wa kupokonya silaha, na kujitolea kamwe kutotumia silaha za nyuklia kwa hali yoyote.
  3. Na Leo, ili kusaidia kulinda afya ya Watoto, Shirika la Umoja wa Matafa la Afya Ulimwenguni limetoa machapisho mawili mapya, “Uhuru dhidi ya tumbaku na nikotini: mwongozo kwa shule,” na “zana za shule zisizo na nikotini na tumbaku.” Lengo la machapisho hayo ni kuzuia hali ambayo inazidi kuenea ya matumizi ya sigara hasa za kielektroniki kwa vijana hasa wanafunzi.
  4. Katika mashinani Samuel Eto’o Rais wa shirikisho la soka Cameroon anasema mchezaji atamulika mbinu za kuepusha soka kutumika kusafirisha kiharamu binadamu.

Mwenyeji wako ni Flora Nducha, karibu!

Audio Credit
Flora Nducha
Audio Duration
11'49"