Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

TANBAT 6, Walinda amani wa UN kutoka Tanzania wapokea pongezi kutoka JWTZ na MINUSCA 

TANBAT 6, Walinda amani wa UN kutoka Tanzania wapokea pongezi kutoka JWTZ na MINUSCA 

Pakua

Walinda amani wa Umoja wa Mataifa Kikosi cha 6 cha kutoka Tanzania TANBAT 06 wanaohudumu chini ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati (MINUSCA) wamepokea ugeni na salamu kutoka Jeshi la Ulinzi wa Wananchi Tanzania (JWTZ) kupitia ujumbe uliongozwa na Brigedia Jenerali George Mwita Itang’are aliyewakilisha salamu za Mkuu wa Majeshi ya Tanzania kutokana na sifa nzuri anazozipokea kutoka MINUSCA kuhusu kikosi hicho. Kutoka mjini Berbérati mkoani Mambéré-Kadéï, Afisa Habari wa TANBAT 06 Kapteni Mwijage Inyoma ameshiriki mapokezi ya ugeni huo, anaripoti.  

Kwanza ni gwaride la ukaguzi…na kisha baadaye ukumbini ni nyimbo za morali. Brigedia Jenerali Itangare katika ziara hii aliyoambatana na Brigedia Jenerali Robert William Mtafungwa ambaye ni Mwambata Jeshi katika Uwakilishi wa kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa akizungumza na maafisa na askari walinda amani baada ya ziara yake ya kutembea kikosi hicho amesema kuwa lengo la ziara ya ujumbe huo ni kuangalia utayari wa kikosi lakini pia kuwapongeza kwa kazi nzuri na utayari pale wanapopewa jukumu.  

Aidha Brigedia Jenerali Itang’are amewataka walinda amani hao kuzingatia maadili ili wasiuchafue Umoja wa Mataifa, Jeshi la Tanzania na taifa lao.  

Kwa upande wake Mkuu wa TANBAT 06 Luteni Kanali Amini Stephen Mshana ameshukuru Jeshi la Tanzania kufanya ziara ya kutembelea kikosi hicho nchini CAR lakini pia akawakumbusha askari  yaliyozungumzwa amehahidi kuendeleza mafanikio waliyoyaona ikiwemo kutekeleza maelekezo ambayo wameyapokea.  

Audio Credit
Kapteni Mwijage Inyoma
Audio Duration
3'42"
Photo Credit
TANBAT 6/Kapteni Mwijage Inyoma.