Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kikosi cha Tanzania TANZBAT6 watoa huduma ya maji kwa wananchi nchini CAR

Kikosi cha Tanzania TANZBAT6 watoa huduma ya maji kwa wananchi nchini CAR

Pakua

Kikosi cha sita cha walinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Tanzania wanaohudumu chini ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati – MINUSCA wametoa huduma ya maji safi na salama kwa vijiji vinavyokabiliwa na uhaba wa maji mjini Berberati mkoa wa Mambéré-Kadéï. 

Siku ya leo ni shangwe isiyo na kifani kwa wananachi wa kijiji cha Savaderi Kilichoko mkoani Mambéré-Kadéï baada ya kikosi cha TANZBAT6 kutoa msaada wa kuwagawia maji waliyobeba kwenye magari yao maalum.

Wananchi hawa wanakabiliwa na changamoto kubwa ya upatikanaji wa maji safi na salama. Afisa jamii na walinda amani kutoka Tanzania Luteni Alyoice Tyraphone  Deusi, kwa niaba ya Mkuu wa TANZBAT06 Luteni kanali Amin Stephen Mshana, baada ya kutoa huduma hiyo ya maji katika vijiji kadhaa akasema wameona ni njia rahisi ya uhusiano bora na jamii.

Kwa upande wake Bi Christin Mamaduu, mmoja wa akina mama wa eneo hilo baada ya kutua ndoo ya maji kichwani alitoa shukrani zake kwa walinda amani kutoka Tanzania chini ya MINUSCA.

 “Tunashukuru sana kwa walinda amani kutoka Tanzania kwa jinsi walivyo amua kutupa msaada wa maji safi hapa nyumbani maana hatuna maji safi hapa kwetu. Huwa tunapata maji ya bomba mara mbili tu kwa wiki na huwa tunanunua. Watu tunakuwa wengi sana, wanasukumana mpaka kuumia. Lakini leo tunajisikia amani kupata maji bila fujo yeyote. Mungu awabariki walinda amani wa Tanzania kwa upendo wao wanaouonyesha hapa kwetu."

Audio Credit
Leah Mushi
Audio Duration
2'27"
Photo Credit
TANBAT6/Kapteni Mwijage Iyoma