Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO yazindua mkakati kutokomeza malaria katika nchi 25 ifikapo 2025 

Shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO yazindua mkakati kutokomeza malaria katika nchi 25 ifikapo 2025 

Pakua

Katika kuelekea  siku ya malaria duniani, inayoadhimishwa kila mwaka tarehe 25 Aprili,  shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO limepongeza idadi kubwa ya nchi zinazokaribia na kufikia, utokomezajhji kabisa wa malaria. Taarifa ya Jason Nyakundi inaeleza kwa kina.

Mpango mpya uliozinduliwana shirika hilo unakusudia kusitisha maambukizi ya ugonjwa huo katika nchi 25 zaidi ifikapo mwaka 2025. 

Ripoti ya WHO inasema kati ya nchi 87 zilizo na malaria, 46 ziliripoti chini ya visa 10,000 vya ugonjwa huo mwaka 2019 ikilinganishwa na nchi 26 mwaka 2000.  

Kufikia mwisho mwa mwaka 2020, nchi 24 ziliripoti kufanikiwa kudhibiti usambaaji wa malaria kwa miaka 3  mfululizo au zaidi na kati ya nchi hizo 11 zilithibitishwa na WHO kutokomeza malaria kabisa. 

"Nchi nyingi tunazozitambua leo zilibeba wakati mmoja mzigo mkubwa sana wa malaria. Mafanikio yao yalipatikana kwa juhudi kubwa na za miongo mingi ya hatua kadhaa. Kwa pamoja, wameuonyesha ulimwengu kuwa kutokomeza malaria ni lengo linalowezekana kwa nchi zote." amesema Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus, mkurugenzi mkuu wa WHO. 

Chachu ya mafanikio 

Ijapokuwa safari ya kila nchi ya kuondokana na malaria ni ya kipekee, chachu ya mafanikio imeonekana katika nchi zote. 

"Mafanikio yanaletwa, kwanza kabisa na kujitolea kwa kisiasa ndani ya nchi yenye ugonjwa wa malaria ili kuumaliza ugonjwa huo. Kujitolea huku kunatafsiriwa kutokana na ufadhili wa ndani ambao mara nyingi unadumishwa kwa miongo mingi hata baada ya nchi kutokuwa na visa vyovyote vya malaria" amesema Dk Pedro Alonso, Mkurugenzi wa mpango wakudhibiti malaria duniani wa WHO 

Kwa mujibu wa WHO nchi nyingi ambazo zinafikia kiwango cha kutokomeza kabisa malaria zina mifumo madhubuti ya huduma ya afya ambayo inahakikisha upatikanaji wa kinga ya malaria, utambuzi na huduma za matibabu, bila kukabiliwa na shida za kifedha, kwa kila mtu anayeishi ndani ya mipaka ya nchi hiyo bila kujali utaifa au hadhi ya kisheria. 

Shirika hilo limesema sababu nyingine kubwa ya mafanikio ni mifumo bora ya takwimu, na ushirikishwaji wa jamii. 

Nchi nyingi ambazo zinatokomeza malaria zinategemea mitandao imara ya wahudumu wa afya wanaojitolea kubaini na kutibu ugonjwa huo katika maeneo ya vijijini n ahata yale ambayo ni vigumu kufikika. 

Mama na mwanae wa umri wa miezi tisa wakilala chini ya neti iliyotolewa na UNICEF kwenye jimbo la Upper Nile, Sudan Kusini.
© UNICEF/Mark Naftalin
Mama na mwanae wa umri wa miezi tisa wakilala chini ya neti iliyotolewa na UNICEF kwenye jimbo la Upper Nile, Sudan Kusini.

Ripoti mpya:kukaribia kutokomeza malaria 

Kupitia mpango wa E-2020, uliozinduliwa mwaka 2017, WHO imesaidia nchi 21 katika juhudi zao za kutokomeza malaria ndani ya ratiba ya mwaka 2020.  

Ripoti mpya ya WHO inaelezea kwa muhitasari hatua zilizopigwa na yale ya kujifunza kutoka  katika nchi hizi katika kipindi cha miaka 3 iliyopita. 

Ripoti inasema nchi 8 kati ya nchi wanachama wa E-2020 ziliripoti kutokuwa na wagonjwa wowote wa malaria ilipofika mwishoni mwa mwaka 2020, ambazo ni Algeria, Belize, Cabo Verde, China, El Salvador, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Malaysia na Paraguay.  

Nchi zingine kadhaa zimeelezwa kupiga hatua kubwa ikiwemo Timor-Leste ambayo iliripoti kisa 1 tu, wakati nchi zingine tatu  ambazo ni Bhutan, Costa Rica na Nepal ziliripoti wagonjwa chini ya 100. 

Kuendeleza mafanikio hayo ya E-2020, WHO imebaini kikundi kipya cha nchi 25 ambazo zina uwezo wa kumaliza malaria katika kipindi cha miaka 5.  

Kupitia mpango wa E-2025, uliozinduliwa wiki hii nchi hizi zitapata msaada maalum na mwongozo wa kiufundi zinapofanya kazi kufikia lengo la kutokomeza kabisa ugonjwa wa malaria. 

Kutokomeza malaria ni mafanikio makubwa 

Katika kukabiliwa na tishio linaloendelea la dawa ya malaria kuwa sugu , nchi zinazosumbuliwa na tatizo hilo katika ukanda wa Asia kwenye baadhi ya majimbo zimepiga hatua kubwa kuelekea lengo lao la pamoja la kutokomeza malaria ifikapo mwaka 2030. 

Katika nchi 6 za eneo hilo zikiwemo Cambodia, China (katika mkoa wa Yunnan), Jamhuri ya Kidemokrasia ya watu wa Lao, Myanmar, Thailand na Viet Nam idadi iliyoripotiwa ya visa vya malaria ilipungua kwa asilimia 97% kati ya mwaka 2000 na 2020.  

Vifo vya Malaria vilipunguzwa kwa zaidi ya asilimia 99% katika kipindi hicho hicho kutoka vifo 6000 hadi vifo 15. 

Kupambana na malaria wakati wa COVID-19 

Mwaka 2020, COVID-19 iliibuka kama changamoto kubwa katika vita dhidi ya malaria ulimwenguni.  

Tangu siku za mwanzo za ugonjwa huo, WHO ilizitaka nchi kudumisha huduma muhimu za afya, pamoja na za kupambana na ugonjwa wa malaria, huku zikihakikisha kuwa jamii na wahudumu wa afya wanalindwa kutokana na maambukizi ya COVID-19. 

Kwa kuitikia wito huo, nchi nyingi zilizo na ugonjwa wa malaria zilichukua hatua Madhubuti na bunifu zikibadilisha njia ya kupeleka huduma za malaria kutokana na vizuizi vya COVID-19 vilivyowekwa na serikali imesema ripoti hiyo ya WHO. Kutokana na juhudi hizi, hali mbaya iliyotarajiwa na WHO imeweza kuepukwa. Uchunguzi ulibaini kuwa ikiwa upatikanaji wa vyandarua vya mmbu na dawa za malaria vitapunguzwa sana, idadi ya vifo vya malaria Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara ingeweza kuongezeka mara mbili 2020 ikilinganishwa na 2018. 

 Pamoja na hilo ikiwa ni zaidi ya mwaka mmoja katika janga hilo, usumbufu mkubwa kwa huduma za afya unaendelea kote ulimwenguni.  

Kulingana na matokeo ya utafiti mpya wa WHO, takriban theluthi moja ya nchi zote duniani ziliripoti usumbufu katika harakati zake za kuzuia malaria, kubaini ugonjwa huo na huduma za matibabu wakati wa robo ya kwanza ya 2021. 

 Katika nchi nyingi, sheria za kusalia majumbani na vizuizi vya kusafiri watu na bidhaa vimesababisha ucheleweshaji wa utoaji wa vyandarua vilivyotiwa dawa za kuzuia mmbu au kampeni za kunyunyizia dawa za kuua wadudu majumbani.  

Huduma za uchunguzi na matibabu ya malaria zilikatizwa kwani watu wengi hawakuweza au hawakutaka  kwenda kupata huduma katika vituo vya afya. 

WHO inatoa wito kwa watu wote wanaoishi katika nchi zilizoathiriwa na malaria "kuishinda hofu” na watu walio na homa wanapaswa kwenda kwenye vituo vya afya karibu nao kupimwa malaria na kupata huduma wanayohitaji, kulingana na itifaki za kitaifa za COVID-19. 

Changamoto Afrika 

Kwa mujibu wa mkurugenzi wa kanda ya afrika wa WHO Dkt. Matshidiso Rebecca Moeti amesema ingawa ukanda wa Afrika ndio unaoongoza kwa asilimia 94 ya vifo na wagonjwa wa malaria umepiga hatua kubwa katika vita dhidi ya ugonjwa huo na katika juhudi za kuelekea kuutokomeza kabisa ugonjwa wa Malaria unaokattili maisha ya watu wengi zaidi ya ugonjwa mwingine wowote. 

Ameongeza kuwa katika miongo miwili iliyopita zaidi ya visa bilioni 1.2 vya malari na vifo milioni 7.1 vimeweza kuepukwa na Aligeria imefanikiwa kutokomeza kabisa gonjwa hili huku nchi kama Botswana, Ghana, Gambia, Namibia, Ethiopia na Afrika Kusini walitimiza lengo la mwaka 2020 la kupunguza malaria kwa kiasi kikubwa.  

Hata hivyo amesema pamoja na mafanikio hayo bado kuna changamoto kubwa. “Kila mwaka tunapoacha malaria iendelee kusambaa afya na maendeleo vinaathirika. Malaria ni chanzo cha kupunguza ukuaji wa uchumi barani Afrika kwa asilimia 1.3 kila mwaka, watu wanaoshindwa kuhudhuria kazi kutokana na malaria mathalani nchini Nigeria wanaleta hasara inayokadiriwa kuwa ni ya dola bilioni 1.1 kila mwaka.” 

Ili kushughulikia changamoto hizo za kijamii na kiuchumi amesema lazima hatua madhubuti na za gharama nafuu zichukuliwe na kuzifikia jamii zilizo hatarini zaidi kwani  “Kuanzia mwaka 2019 kaya 1 kati ya 3 kwenye ukanda huu hazikuwa na vyandarua vya mbu vyenye dawa, na karibu nusu ya watoto wote wa chini ya umri wa miaka 5, hawakulala kwenye vyandarua, theluthi mbili ya wanawake wajawaziti hawakupata tiba yak inga ya malaria na kwa kukosa ulinzi huo zaidi ya wanawake milioni 11 wajawazito walipata malaria na watoto zaidi ya laki nane walizaliwa na uzito mdogo.” 

Kwa mantiki hiyo amesema ubunifu utakuwa muhimu sana ili kufikia lengo la kutokomeza malaria ikiwemo upatikanaji wa chanjo dhidi ya ugonjwa huo. 

“Hivyo tunahamasa kubwa kwamba Kenya, Ghana na Malawi wametoa zaidi ya dozi milioni 1.7 za chanjo. Hii ni nyenzo ya ziada inayotia matumaini katika kuzuia malaria.” 

Audio Credit
Grace Kaneiya/Jason Nyakundi
Audio Duration
3'36"
Photo Credit
Sven Torfinn/WHO 2016