Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Volkan Bozkir: Baraza Kuu la mwaka huu ni la kipekee kwa namna nyingi

Volkan Bozkir: Baraza Kuu la mwaka huu ni la kipekee kwa namna nyingi

Pakua

Rais mpya wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kikao cha 75 Volkan Bozkir amesema kikao cha mwaka huu cha Baraza Kuu ni cha kipekee kwa namna nyingi, kwani mbali ya janga la corona au COVID-19 , Umoja wa Mataifa unatimiza miaka 75 tangu kuanzishwa. Jason Nyakundi na maelezo zaidi.

Bwana Bozkir mwanadiplomasia nguli kutoka nchini Uturuki anapokea kijiti cha kuongoza kikao cha 75 katika hali isiyo ya kawaida wala ya kutarajiwa. Mwanadiplomsia huyo mwenye uzoefu wa karibu miaka 50, amekuwa mfanyakazi wa umma na hivi karibuni alikuwa waziri wa masuala ya Ulaya na alichaguliwa kutoka kundi la Ulaya Magharibi na wengine kwenye Umoja wa Mataifa , na sasa anachukua nafasi ya Tijjani Muhammad-Bande kutoka nchini Nigeria. 

Bwana Bozkir alijiunga na wizara ya mambo ya nje ya Uturuki mwaka 1972 na ameshikilia nyadhifa mbalimbali za kidiplomasia ikiwemo kuwa balozi wa Uturuki kwenye Umoja wa Mataifa mjini New York, pia aliwahi kuwa balozi Bucharest na mwakilishi wa kudumu wa Uturuki kwenye Muungano wa Ulaya. 

Akizungumza na UN News kabla ya kuanza rasmi kikao cha 75 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa wiki hii amesema atafanya nini ili kuhakikisha jamii na watu walio hatarini watalindwa na jinsi atakavyokabiliana na changamoto zilizoletwa na janga la corona au COVID-19, “bila shaka janga la COVID-19 limekuwa ndio kipaumbele kikubwa na kinachotiliwa mkazo hivi sasa , ndio maana nimeamua kupitisha mada ya kikao cha 75 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, mada iliyochaguliwa na nchi wanachama ya mustakabali tunaoutaka, Umoja wa Mataifa tunaoutaka:ikisisitiza jukumu letu la pamoja katika kudumisha ushirikiano wa kimataifa. Nikaongezea juu ya hapo kukabiliana na COVID-19 kupitia hatua za pamoja za kimataifa kwa sababu , janga hili linazijaribu taasisi zetu kuliko wakati mwingine wowote , tuna wajibu wa kuchukua hatua katika ngazi ya kimataifa kukabili virusi hivi na changamoto inazozileta katika uchumi wetu na jamii.” 

Na alipoulizwa kuhusu maadhimisho ya miaka 75 ya Umoja wa Mataifa akiwa kama Rais wa Baraza Kuu inamanisha nini, mwanadiplomasia huyo amesema, “COVID-19 ni mgogoro wa kimataifa ambao dunia haijaushuhudia tangu kuundwa kwa Umoja wa Mataifa kutoka kwenye majivu ya vita vikuu vya pili vya dunia. Sio tu kwamba ni mgogoro wa kiafya lakini pia ni mgogoro wa kijamii na kiuchumi ambao umezidisha ugumu wa changamoto zilizokuwepo ambazo Umoja wa Mataifa unajaribu kuzitatua kupitia ajenda ya 2030 ya maendeleo endelevu na malengo ya maendeleo endelevu. Binadamu wote wako katika vita hivi pamoja. Ni wakati wa umoja, nchi wanachama hazijawahi kuwa na sababu muhimu ya kufanyakazi pamoja kwa ajili ya maslahi ya pamoja kama sasa. Na nina uhakika kwamba kwa pamoja tutalishinda janga hili tukiwa na nguvu” 

Ameongeza kuwa katika yote haya Umoja wa Mataifa na hususan Baraza Kuu lina jukumu muhimu. Kupitia chombo hiki nchi wanachama wameweka kanuni na wanaelekeza rasilimali zetu za pamoja kushughulikia changamoto za pamoja.  

Chanjo mathalani, je chanjo ya COVID-19 itakuwa ni suala la kimataifa la pamoja itakayogawiwa kwa usawa? "Huu ni ugonjwa usioheshimu mipaka ya kitaifa. Hatuko salama hadi kila mtu atakapokuwa salama." Amesema mwanadiplomasia huyo.

Rais mteule wa mkutano wa 75 wa Baraza Kuu la UN, Volkan Bozkir (kushoto) katika picha ya pamoja na Katibu Mkuu wa UN António  Guterres katika picha hii ya pamoja ya Januari 2020.
UN /Manuel Elias
Rais mteule wa mkutano wa 75 wa Baraza Kuu la UN, Volkan Bozkir (kushoto) katika picha ya pamoja na Katibu Mkuu wa UN António Guterres katika picha hii ya pamoja ya Januari 2020.

 

Mabadiliko ya UN na jinsi ya kuendelea kuwa na maana miaka 75 ijayo 

Kuhusu mabadiliko na Umoja wa Mataifa kuendelea kuwa na maana katika miaka 75 ijayo, Rais huyo mpya wa Baraza Kuu amesema, “maadhimisho haya ya kihistoria ni fursa ya kipekee ya kutafakari yaliyopita na kile ambacho tayari kimefikiwa na kendeleza mafanikio hayo ili kuzishinda changamoto za sasa zinazokabilia mshikamano wa kimataifa na Umoja wa Mataifa” 

Amesisitiza kwamba taasisi zinapaswa kwenda sanjari na wakati na kujifanyia mabadiliko ili ziweze kuendelea kuwa na maana. Naunga mkono ajenda ya mabadiliko ya Umoja wa Mastaifa na mabadiliko tuliyoyashuhudia katika nyanja za amani na usalama, maendeleo na utawala. Hatua hizi ni muhimu katika kuifanya familia nzima ya Umoja wa Mataifa kushikamana na kuungana.  

Amekumbusha kwamba Umoja wa Mataifa hadi leo hii ndio shirika pekee lenye wanachama wa kimataifa ambalo linaanzisha kanuni za kukabiliana na matatizo ya kimataifa kupitia ushirikiano wa kimataifa. 

Na Baraza Kuu ndio chombo pekee cha Umoja wa Mataifa ambacho nchi wanachama wote wana sauti sawa. 

Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa na sehemu ya majengo marefu ya Manhattan, 24 Oktoba 1955
UN Photo.
Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa na sehemu ya majengo marefu ya Manhattan, 24 Oktoba 1955

 

Kwa nini makundi na walio hatarini ni kipaumbele 

Rais Bozkir amesema changamoto za kimataifa na migogoro huathiri zaidi nchi na watu walio hatarini,  “watu wenye mahitji au ambao wako chini ya ukandamizwaji wanapaswa kuhisi kwamba hofu zao zinasikilizwa kwenye chmbo cha Umoja wa Mataifa ambacho ni cha kidemokrasia zaidi. Nitafanyakazi kuhakikisha naleta sauti za watu wa dunia kwenye majadiliano yetu. Kusongesha ajenda ya kibinadamu ya umoja wa Mataifa kwa kuzingatia walio hatarini zaidi hilo ndilo litakuwa kitovu cha Urais wangu.” 

Mwaka 2020 ni muhimu kwa haki za wanawake 

Mwaka 2020 ni mwaka muhimu kwa haki za wanawake , kwani ni maadhimisho ya 25 tangu kupitishwa kwa azimio la jukwaa la hatua la Beijing na ni maadhimisho ya 20 ya azimio la kihiostoria la Baraza la Usalama kuhusu wanawake, amani na usalama. Je ni hatua gani atakazozichukua Bozkir kuhakikisha uwezeshaji wa wanawake na wasichana? 

Rais mpya wa Baraza Kuu kuhusu hilo amesema ushahidi unaonesha kwamba usawa wa kijinsia unasaidia katika kiwango kikubwa cha amani na mafanikio,“wanawake mara nyingi wanakosa fursa za kupata ajira zenye hadhi, ujira sawa, elimu bora na huduma za kutosha za afya. Wanaathirika na ukatili na ubaguzi na mara nyingi hawawakilishwi vya kutosha katika mchakato wa maamuzi ya kisiasa na kiuchumi. Na kwa bahati mbaya kwa kusambaa kwa janga la COVID-19 hata mafanikio yaliyopatikana katika miongo iliyopita sasa yako hatarini. hilo ni lazima libadilike.” 

Amesema kuwa kuboresha maisha ya wanawake kunazifanya jamii kuwa jumuishi na zenye ufanisi jambo ambalo linamsaidia kila mtu. Amesema kama taasisi ambayo kimsingi inaweka viwango vya kimataifa, Umoja wa Mataifa unapaswa kuongoza kwa mfano, "Kwa upande wangu nimetoa kipaumbele maalum katika usawa wa kijinsia wakati naunda timu yangu, ambayo sasa inajumuisha wanawake wengi kuliko wanaume na ina uwiano wa kijinsia katika uongozi wa juu. Na nitahakikisha kwamba lenzi za jinsia zitatumika katika kazi tunazozifanya katika masuala ya amani na usalama, haki za binadamu, masuala ya kibinadamju na maendeleo endelevu.” 

Nini kilikushawishi kuwania Uraia wa GA 

Nini kilimshawishi au kumuhamasisha Rais huyu wa kikao cha 75 kuingia katika kinyang’anyiro cha nafasi hiyo? Bwa, Bozkir anasema “kama mwanadiplomasia nguli na mwanasiasa kwa karibu miaka 50, nimetumia maisha yangu yote wa kitaaluma katika huduma za umma. Ilikuwa chachu ya hamasa yangu ya kuhudumia nchi na taifa langu.” 

Na kwa sasa anasema “niko katika mwanzo mpya na ukurasa mpya ambao ninajivunia ambapo nitakuwa nawahudumia nchi zote wanachama wa Umoja wa Mataifa . Kilichonihamasisha kuchukua jukumu hili ambalo ni changamoto mpya ni imani yangu kubwa katika ufanisi wa ushirikiano wa diplomasia ya kimataifa, na pia nia yangu ya kuhudumia na kuchangia hata kama ni kidogo katika historian a kwa ustawi wa binadamu wote. Siwezi kufikiria pengine popote pa kufanya hayo ispokuwa kwenye Umoja wa Mataifa.” 

 

 

  

Audio Credit
Flora Nducha/Jason Nyakundi
Sauti
3'40"
Photo Credit
UN /Manuel Elias