Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COVID-19 yaongeza machungu sekta ya utalii Kenya

COVID-19 yaongeza machungu sekta ya utalii Kenya

Pakua

Janga la ugonjwa wa virusi vya Corona, COVID-19 nchini Kenya limekuwa na athari kwa sekta ya uhifadhi wa wanyamapori na hivyo kuweka hatarini mustakabali wa wanyamapori kwenye hifadhi. Flora Nducha na ripoti kamili. 

Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa, UNEP kupitia video yake limemulika hifadhi ya taifa ya Amboseli, kusini mwa Kenya ambayo tangu COVID-19 ikumbe taifa hilo katikati ya mwezi Machi mwaka huu,, imesababisha sekta ya utalii kudorora, wakazi jirani wa eneo hilo kukosa ajira na wanyama kukosa ulinzi. 

UNEP inaita hali ya sasa ni janga la uhifadhi kwa kuwa miradi mingi ya ulinzi wa wanyamapori inatokana na mapato ya utalii lakini sasa kutokana na COVID-19, utalii umeporomoka, na kuna hofu ya kwamba ujangili utaongezeka. 

Dickson Pamuya ni miongoni mwa wananchi waliokuwa wanajipatia kipato kwa kutembeza watalii mbugani na kujipatia kipato na anasema,  

“Nimefanya kazi ya kutembeza watalii mbugani kwa zaidi ya miaka minane.Nilijivunia sana kuona watalii wanakuja kutembelea Kenya. Lakini sasa hakuna kazi kwa sababu ya virusi vya Corona. Hakuna matembezi mbugani, hakuna wageni kwa sababu ya COVID-19. Kama hakuna utalii, hakuna uhifadhi.” 

Kwa Jonhson Salaash ambaye awali alikuwa mkulima lakini sasa ni mhifadhi wa kijamii, suala la kujikita zaidi kwenye COVID-19 na kusahau uhifadhi ni tatizo akisema kuwa,  

“Fedha nyingi zimeelekezwa kwenye kukabili COVID-19, na majangili bado wapo, hatua bado zinahitajika kuwakabili, na kama hakuna fedha, hii itakuwa ngumu zaidi. “ 

Doreen Robinson, Mkuu wa masuala ya wanyamapori UNEP anasema madhara ya COVID-19 kwa wanyama ni makubwa, 

 “Hivi sasa hakuna tena mapato, watu hawana fedha za kununua chakula, na watu wanaoishi karibu na mbuga ndio walinzi wa kwanza wa wanyamapori, na hofu yetu ni kwamba watu wanakuwa na hofu na watatamani kuvamia hayo maeneo ili kukidhi mahitaij yao ya msingi. Kwa hiyo UNEP hivi sasa inashirikiana na nchi nyingi  kupanua wigo wa uchumi utokanao na wanyamapori. Ili uhifadhi wa wanyamapori uwezekane, watu wanapaswa kunufaika na kufurahia maliasili.” 

Audio Credit
Assumpta Massoi\Flora Nducha
Audio Duration
2'9"
Photo Credit
UN /John Isaac